Waziri Damas Ndumbaro aiokoe Majimaji FC

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro.

Agosti 30, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, kuna waliohamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine, wapo ambao waliteuliwa kwa mara ya kwanza lakini pia wengine walibakia katika wizara walizokuwepo mwanzoni.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyoteka hisia za wengi ni yale yaliyofanywa katika wizara ya utamaduni, sanaa na michezo ambapo aliyekuwa waziri wake, Pindi Chana alihamishwa kupelekwa wizara ya katiba na sheria.

Na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alihamishiwa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Wadau wengi wa michezo wameyatazama na kuyapokea mabadiliko hayo ya kuletewa Dk Ndumbaro kwa hisia chanya na matumaini makubwa kutokana na waziri huyo kuwa miongoni mwa watu ambao wamekuwa na msaada mkubwa michezoni hasa kwenye soka.

Kwa nyakati tofauti, Dk Ndumbaro alishika nyadhifa tofauti za kimichezo, ndani ya nchi lakini pia katika mkoa wake wa Ruvuma.

Lakini kana kwamba haitoshi, yeye ni miongoni mwa wachezaji wa gofu wazuri hapa nchini na mara kadhaa amekuwa akionekana akishiriki katika kuucheza.

Kwa vile amekuwa na ufahamu mkubwa wa michezo kwa kuongoza au kusaidia ipige hatua kwa kuchangia fedha, vifaa, huduma na ushauri, ndoto ya wanamichezo wengi ni kuona nyanja hiyo inapata maendeleo makubwa zaidi chini yake.

Hata hivyo, wakati Dk Ndumbaro akiteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo ambayo inasimamia jambo linalopendwa na kundi kubwa la watu tofauti, jimboni kwake Songea Mjini kuna maumivu ya mashabiki wa mpira wa miguu kutoona mechi za madaraja ya juu ya ligi hapa nchini kwa maana ya Ligi Kuu na Ligi ya Champioship.

Hii ni kwa sababu timu iliyokuwa inawawezesha kutimiza lengo hilo ya Majimaji, kwa sasa haipo kwenye madaraja hayo na hata lile la First League kutokana na kushuka daraja ambako kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na changamoto za kiuchumi.

Timu hiyo ilijikuta ikishindwa kusafiri kwenda katika kituo cha mchezo kwa baadhi ya mechi na hivyo kujikuta ikikatwa idadi kubwa ya pointi ambazo ingekuwa nazo pengine ingeweza kujinusuru na kubakia.

Wahenga walisema kujitolea kunaanzia nyumbani hivyo katika kipindi hiki ambacho anakuja katika wizara inayohusika na michezo, Dk Ndumbaro anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kurudisha furaha ya Wanasongea kwa Majimaji.

Haimaanishi kuwa atumie nafasi yake kulazimisha mamlaka za soka ziirudishe Majimaji kati ngazi za juu za ligi bali asaidie iweze kupata mahitaji yake muhimu ambayo yataitengenezea urahisi wa kupanda.

Kwa nafasi yake awaunganishe Wanasongea na wote wenye nia ya kuona mkoa wa Ruvuma unakuwa na timu katika madaraja ya juu ya ligi, wajitoe kwa hali na mali ili furaha yao iweze kurejea.

Inawezekana ndani ya Majimaji kuna changamoto nyingi ambazo zimemfanya Waziri Ndumbaro ajiweke kando na timu hiyo, lakini hayo anapaswa kuyasamehe na kuanza upya kwa faida ya nyumbani ambako pia ni jimboni kwake.

Kitendo cha Majimaji kufanya vizuri na kufika juu, ukiachana na kusaidia watu wa Songea kiuchumi lakini pia hata kwa Waziri mwenyewe ni mtaji ambao utamuweka katika nafasi nzuri ya kutetea kiti chake siku za usoni.

Na kwa mashabiki wa Majimaji na watu wa Songea kiujumla, mnapaswa kuhakikisha mnamtumia Waziri Ndumbaro kwa kushirikiana naye vyema ili heshima ya Majimaji iweze kurejea.

Maneno maneno na majungu ambayo yanamfanya arudi nyuma yeye au wadau wengine yanapaswa kuepukwa na wote mnatakiwa kuimba wimbo mmoja.

Tabia hii ipo katika mikoa mingi na timu zinashindwa kurudi kwenye Ligi Kuu kutokana na baadhi ya watu kuamini kuwa bila wao hakuna kitu kinaweza kufanyika au kusukuma gurudumu la maendeleo ya soka kwa eneo husika.

Hii imetokea kwa mikoa mingi kama Mwanza na Arusha pia, ambako kuliwahi kuwa na timu za Ligi Kuu, lakini mambo yamekuwa tofauti kwa sasa na hakuna maendeleo.

Arusha kuliwahi kuwa na AFC na JKT Oljoro, lakini kwa sasa imebaki kuwa historia. Mara kadhaa AFC ilitaka kunyanyuka lakini inakumbana na wakati mgumu wa kufikia malengo.

Hali hiyo ipo pia katika klabu za Mwanza, ambazo bado hazijapata unafuu wa kutoka Daraja la Kwanza (Championship) kurudi zilipokuwa, kama Toto Africans na Mbao FC.