Miaka 17 Mv Bukoba, tumepata mafunzo gani?

Muktasari:

Tangu kutokea kwa ajali hiyo kumekuwa na mwendelezo wa ajali za majini katika sehemu mbalimbali nchini na hasa katika Bahari ya Hindi. Hatujasahau meli ya Mv Skagit iliyozama kwenye bahari hiyo na miongoni mwa sababu ikiwa ni kujaza abiria kupita kiasi.

Jana imetimia miaka 17 tangu kutokea kwa ajali ya meli ya Mv Bukoba iliyozama alfajiri ya Mei 21, 1996 umbali wa kilomita chache kutoka Bandari ya Mwanza na kusababisha vifo vya zaidi ya abiria 1,000.

Watanzania kila mwaka wamekuwa wakiadhimisha kumbukumbu ya vifo vya ndugu na jamaa zao waliopoteza maisha kwa kuzama na meli hiyo, iliyokuwa ikitokea Bukoba mkoani Kagera kwenda Mwanza.

Ni kumbukumbu yenye machungu kwa kuwa sababu za ajali hiyo kwa asilimia kubwa ni uzembe wa kuruhusu meli hiyo kufanya kazi wakati ikiwa mbovu na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi.

Meli hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Ubelgiji ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 850 za mizigo na abiria 430. Lakini ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa ajali hiyo iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga ilisema siku ya ajali, meli hiyo ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37.

Tangu kutokea kwa ajali hiyo kumekuwa na mwendelezo wa ajali za majini katika sehemu mbalimbali nchini na hasa katika Bahari ya Hindi. Hatujasahau meli ya Mv Skagit iliyozama kwenye bahari hiyo na miongoni mwa sababu ikiwa ni kujaza abiria kupita kiasi.

Ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo ilibainisha kuwa Mv Skagit iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 230, wakati wa ajali ilikuwa na abiria karibu 400 na mizigo.

Vilevile kuna ajali ya Mv Spice Islander iliyotokea Septemba 10, 2011 eneo la Nungwi, Kaskazini Unguja iliyokuwa imebeba abiria 2,470 badala ya 620 tu, huku ikielezwa kuwa pia iliripotiwa ni mbovu miezi miwili kabla ya kuzama.

Wakati miaka ikizidi kupita tangu kuzama kwa Mv Bukoba, matukio ya kuzama kwa vyombo vya majini yamekuwa yakiongezeka na juhudi za kuyadhibiti zinaonekana kuwa bado ni ndogo.

Bahati nzuri matukio hayo yanapotokea, hasa yale makubwa, miongoni mwa sababu zinazotajwa ni ubovu wa vyombo hivyo na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi. Kwa maana nyingine ni sababu zinazoweza kuzuilika.

Hata yale mapendekezo ya kuandaa wataalamu wetu wa uokoaji wenye uwezo wa kuzamia kwenye maji ya kina kirefu hayajafanyiwa kazi, kwani tumeshuhudia kila mara wanasubiriwa wataalamu wa nje, hali inayochangia ongezeko la vifo vya abiria.

Mwaka 2004 Serikali ilipitisha sheria iliyounda Sumatra, ambayo kazi yake kuu ni kudhibiti vyombo vya usafiri nchikavu na majini, lakini kutokana na matukio hayo ni wazi haijakidhi haja ya kuwapo kwake, kwa kuwa bado kuna uzembe wa udhibiti wa vyombo hivyo.

Uzembe huo umeendelea kuwa wazi na hatuoni ukaguzi wa kuridhisha wa vyombo vyote vinavyosafirisha abiria majini, ili kuhakikisha vinakuwa katika hali ya usalama na vinabeba abiria na mizigo kadri ya uwezo wake.

Hatujasikia meli yoyote ikizuiwa na abiria wake kuteremshwa au mizigo kupunguzwa kutokana na kuzidisha idadi na uzito au kutokana na ubovu wake licha ya kwamba hali hiyo inatokea kila siku kwenye vyombo vyetu.

Hatujaona chombo chochote kikifungiwa au kunyimwa leseni kutokana na kukiuka masharti ya usafirishaji.

Miaka 17 ni mingi, tuseme sasa inatosha. Ni imani yetu kuwa iwapo ingewekwa mikakati ya kuondokana na ajali hizo zinazoweza kuzuilika, tungekuwa tumefanikiwa kudhibiti ajali hizi zinazoua nguvukazi ya taifa.