Umisseta itumike kuibua vipaji, kujenga umoja
Soka kandanda
Muktasari:
Mashindano hayo ya taifa yanaandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Michezo ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) inaendelea kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani na inatarajiwa kumalizika wiki ijayo.
Mashindano hayo ya taifa yanaandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mashindano hayo yalianza kwa kufanyika katika manispaa mbalimbali kwa kugawanywa katika kanda na vijana waliofanya vizuri ndio waliochaguliwa kuiingia kwenye michezo hiyo katika ngazi ya mkoa kwa ajili ya kushindana katika mashindano ya Taifa kwa Shule za Sekondari.
Ni dhahiri kurudishwa kwa michezo hii ya Umisseta sasa tunapata nafasi ya kujenga umoja wa kitaifa wa wanamichezo kupitia michezo hii kuanzia ngazi ya shule za sekondari. Ni kweli michezo ni burudani, lakini kwa sasa kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, michezo ni kipaumbele katika kutoa pia ajira, kukuza biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano.
Kwa mfano, nchi za wenzetu za Ulaya na Marekani, Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon, Algeria zinatumia kikamilifu nafasi hii ya michezo kujitangaza kisiasa na kiuchumi.
Tunatarajia kushuhudia mashindano ya Umisseta mwaka huu yatakuwa na mvuto mkubwa na washiriki wataonyesha kiwango cha juu kwa sababu watakuwa wamejipanga na kuandaliwa vizuri kushiriki kama washindani na sio wasindikizaji.
Tunaamini michezo inatufundisha ushindani wa kistaarabu, ushindani unaozingatia sheria na kanuni, ushindani unaojenga urafiki badala ya uhasama, ushindani unaoleta upendo badala ya chuki na ushindani unaoleta amani badala ya shari. Hivyo tunaamini kushindwa au kushinda ni sehemu ya mashindano na tunaamini asiyekubali kushindwa si mshindani.
Pia, tunaamini wanamichezo bora ni watu wasikivu, wenye nidhamu na watiifu hivyo tunatarajia wanamichezo wote wanaoshiriki katika mashindano hayo ya Umisseta mwaka huu wataonyesha hayo kwa kiwango cha juu.
Ni wazi hatutarajii kusikia maandalizi mabovu ya malazi, chakula na vijana kukosa vifaa vya michezo, dawa, jezi na vinginevyo kwa sababu tunaamini waandaaji wamejipanga ipasavyo.
Pia tunapenda kuwakumbusha vijana wote wanaoshiriki katika mashindano ya Umisseta mwaka kuwa ni lazima wakumbuke kutunza nidhamu yao na kutunza afya zao.
Tunasema hivyo kwa sababu tunaamini vijana wapo Kibaha kwa ajili ya kushindana kimichezo na siyo kujitumbukiza kwenye vitenvyo hatarishi vinavyoweza kusababisha kuambukizwa virusi vya Ukimwi au utumiaji dawa zilizopigwa marufuku.
Vilevile tunatarajia walimu wa michezo waliopo katika mashindano ya mwaka huu watawafuatilia vizuri vijana wote wanaoshiriki ili kuweza kuchagua wachezaji wazuri watakaoendelezwa na kuwa wachezajin wazuri wa michezo mbalimbali na kuwa wabebaji wazuri wa bendera ya taifa kwenye mashindano ya kimataifa.
Kila la heri Umiseta.