Chelsea yatinga nusu fainali Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2014

Chelsea yatinga nusu fainali Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2014

Muktasari:

  • Thomas Tuchel amewashauri wachezaji wake vijana wa Chelsea kuchangamkia safari yao isiyo ya kawaida katika Ligi ya Mabingwa baada ya kufuzu kucheza nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014, licha ya kufungwa bao 1-0 na Porto jana Jumanne katika mechi ya marudiano ya robo fainali.

Seville, Hispania. Thomas Tuchel amewashauri wachezaji wake vijana wa Chelsea kuchangamkia safari yao isiyo ya kawaida katika Ligi ya Mabingwa baada ya kufuzu kucheza nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014, licha ya kufungwa bao 1-0 na Porto jana Jumanne katika mechi ya marudiano ya robo fainali.


Timu ya Tuchel itakutana ama Real Madrid au Liverpool katika nusu fainali kusaka nafasi ya kucheza fainali baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha kudhibiti mchezo jijini Sevilla na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.


Leo Jumatano, Real itakuwa ugenini katika uwanja wa Anfield ikiwania kulinda uongozi wake wa mabao 3-1 ilioupata katika mechi ya kwanza jijini Madrid, ili itinge nusu fainali.


Hawatakiwi wafanye kingine zaidi ya kuiga mbinu za Tuchel zilizoiwezesha Chelsea kuidhibiti Porto kwa mfumo mzuri wa kujilinda kwa muda mrefu kabla ya Mehdi Taremi kufunga bao pekee kwa tik-tak katika dakika ya mwisho ya muda wa majeruhi.


Bao hilo lilikuwa la aina yake kulinganisha na mchezo wa Porto ambayo ilihaha bila ya mafanikio kujaribu kugeuza matokeo ya kipigo cha mabao 2-0 ilichopewa katika mchezo wa kwanza.


Chelsea imepoteza mchezo mmoja tangu Tuchel achukue nafasi ya Frank Lampard aliyetimuliwa Januari na matokeo ya jana yalikuwa kipigo cha pili kwa Mjerumani huyo.


Kufika nusu fainali ni mafanikio makubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba wachezaji wengi katika kikosi cha Tuchel hawana uzoefu na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.


Tuchel anajua wachezaji kama Mason Mount, Reece James, Kai Havertz, Ben Chilwell na Christian Pulisic wanajifunza wakiwa kazini, lakini anatumani kutoogopa kwao kutakuwa muhimu.


"Mason alifunga bao lake la kwanza katika michuano hiyo wakati wa mechi ya kwanza. Wakati Mbappe anapofunga, au Salah au Benzema anapofunga, inakuwa ni bao lao la 100 au la 50 katika mashindano," alisema Tuchel.


"Tulifika tukiwa na timu changa. Wachezaji wanaweza kupambana na kukimbia. Lazima tuchukulie hiki kama safari ya matukio ya maajabu kwao. Ni hatua kubwa.


"Unaona muda tangu Chelsea ifike nusu fainali. Hatujazoea kuwa pale. Ni mafanikio makubwa."