Hesabu muhimu kwa Simba kutinga robo fainali hizi hapa

Mshambuliaji nyota wa Simba, Meddie Kagere akifunga bao mbele ya kipa wa Al Ahly, Mohamed Elshenawy katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ulio-chezwa Dar es Salaam, juzi. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Ushindi wa bao 1-0 iliopata Simba dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa juzi, inaifanya timu hiyo kuamini katika hesabu na mazingira ya mechi za hatua mbili zilizobakia, vinaonekana vitaibeba Simba na kuipeleka hatua ya robo fainali

Hatima ya Simba kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ipo mikononi mwao wenyewe.

Ushindi wa bao 1-0 iliopata dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa juzi, sawa na ule ambao JS Saoura waliupata mbele ya AS Vita yameiweka Simba kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali kupitia kundi D.

Baada ya matokeo ya mechi za juzi, hesabu na mazingira ya mechi za hatua mbili zilizobakia, vinaonekana vitaibeba Simba na kuipeleka hatua ya robo fainali lakini hilo kwa kiasi kikubwa litatokana na jinsi itakavyoweza kuchanga karata zake vizuri.

Kwa sasa Ahly wanaongoza wakiwa na pointi saba, wakifuatiwa na Simba wenye pointi sita, Saoura wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tano huku Vita wakiburuza mkia na pointi zao nne.

Ingawa hadi sasa kila timu kwenye kundi hilo ina nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali kutokana na msimamo ulivyo, Simba na Ahly ndio wanaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kulinganisha na AS Vita na JS Saoura.

Simba ambao mechi ijayo Machi 9, mwaka huu dhidi ya Saoura watakuwa ugenini, wanatakiwa kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya AS Vita utakaochezwa Machi 16.

Wakiibuka na ushindi kwenye mchezo huo, watafuzu robo fainali hata kama watapoteza mechi yao ijayo dhidi ya Saoura.

Hata hivyo, hilo litatokea iwapo AS Vita itaifunga au kutoka sare na Al Ahly kwenye mchezo unaofuata jijini Kinshasa kisha mechi ya mwisho imalizike kwa Saoura kutoka sare au kupoteza ugenini dhidi ya Ahly. Kama kila timu itaibuka na ushindi nyumbani katika raundi mbili zilizobakia, msimamo wa kundi D mwishoni utazibeba Simba na Ahly kwani hatua ya makundi itamalizika, Al Ahly wakiwa na pointi 10, Simba tisa, Saoura watakuwa na pointi nane wakati Vita watakuwa na saba.

Hilo linaonekana lina nafasi kubwa ya kutokea kwani timu hizo zote nne za kundi hilo zimekuwa hazina rekodi nzuri ya kuibuka na ushindi ugenini.

Kwenye mechi tano za mwisho ambazo timu hizo zimecheza ugenini kwenye mashindano ya kimataifa ni Simba tu ambayo imejitahidi kwa kuibuka na ushindi mara moja, kutoka sare moja na kufungwa tatu wakati Saoura, Vita na Ahly zikiwa hazijapata ushindi hata mara moja.

Wakati Al Ahly ikifungwa mechi nne na kutoka sare mara moja katika mechi zake tano za mwisho za mashindano ya klabu Afrika, ikifunga mabao mawili tu na kufungwa manane, AS Vita wao wametoka sare mbili na kufungwa mechi tatu, ikipachika bao moja na kufungwa magoli saba.

Saoura wao katika michezo mitano ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hawajashinda hata mmoja, wametoka sare miwili na kufungwa mitatu huku wakifunga mabao mawili na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara sita.

Lakini Simba wanajivunia rekodi nzuri ya kutumia vyema uwanja wa nyumbani katika mashindano ya kimataifa ambapo katika mechi tano za mwisho walizocheza Uwanja wa Taifa, wameibuka na ushindi mara nne na kutoka sare moja, wamefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili tu.

Hata hivyo Simba wanaweza kuvuka na kuingia robo fainali pasipo kusubiri hata mechi ya mwisho, ikiwa watafanikiwa kuibuka na ushindi wa ugenini dhidi ya Saoura kisha Vita akapoteza au kutoka sare nyumbani mbele ya Al Ahly kwenye raundi ijayo.

Beki na nahodha msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliliambia gazeti hili kuwa ushindi dhidi ya Ahly nyumbani umerudisha morari na hamasa kwa timu yao.

“Wengi walianza kupoteza matumaini baada ya kupoteza mechi zetu mbili zilizopita, lakini baada ya ushindi huu naamini tuna nafasi kubwa ya kusonga mbele,” alisema Tshabalala.

Haijavunja rekodi yake

Simba imekuwa na uwakilishi mzuri katika mashindano ya kimataifa kutokana na hatua mbalimbaliu ilizowahi kufikia na kuweka rekodi nchini.

Rekodi ya kwanza ni kufika hatua ya nusu fainali ya michuoano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na kuwa klabu pekee nchini kufikia hatua hiyo.

Ilifikia hapo baada ya kuitoa klabu ya Hearts of Of Oak ya Ghana katika hatua ya robo fainali kwa jumla ya magoli 2-0.

Hata hivyo, katika nusu fainali licha ya kuanza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Mehala El Kubra ya Misri hapa Dar es Salaam, na kumaliza dakika 90 kwa matokeo kama hayo jijini Cairo, katika mikwaju ya penati mnyama aling’olewa.

Pia, Simba ni klabu pekee ya Tanzania, iliyocheza fainali ya michuano ya kombe la CAF (sasa kombe la Shirikisho) mwaka 1993 na kufungwa 0-2 katika mchezo wa mwisho wa fainali dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Ivory Coast, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

Hata hivyo, licha ya hatua iliyofikiwa na Simba mwaka huu katika michuano hiyo, lakini haijavunja rekodi yake iliyoiweka mwaka 2003 ilipotinga hatua kama hiyo na kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 7.

Moja ya matokeo yaliyowakuna wengi mwaka huo na kuifanya Simba iingie kwenye vitabu vya kumbukumbu ni yale yaliyomng’oa bingwa mtetezi, Klabu ya Zamalek ya Misri.

Simba iliwang’oa mabingwa watetezi hao kwa mikwaju ya penati jijini Cairo baada ya matokeo ya jumla ya mechi iliyochezwa Dar es Salaam na Cairo kuwa 2-2 kila moja ikilala kwa bao 0-1 katika ardhi ya nyumbani.

Mchezo ukalazimika kuamuliwa kwa matuta na Juma Kaseja aliyekuwa golikipa namba moja wa Simba na Taifa Stars aliibeba Simba kwa kuzuia penati mbili.

Katika makundi ilipangwa kundi A lililokuwa na timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Enyimba (Nigeria), Ismaily (Misri) na Simba yenyewe.

Simba ilishinda 1-0 katika mchezo kati yake na Asec Mimosas, ikaifunga Enyimba 2-1 na kutoka suluhu na Ismaily, hivyo ikajikusanyia pointi 7 ambazo kwa msimu huu bado haijazifikia ingawa inayo nafasi ya kufanya hivyo kutokana na kuwa na michezo miwili mkononi mmoja ukiwa ni wa nyumbani dhidi ya AS Vita.

Mwaka huo Enyimba walimaliza wakiwa vinara wa kundi hilo kwa kujikusanyia pointi 12 huku Ismaily ikiwa ya pili na pointi 11 na Asec Mimosaa ilikuwa ya mwisho ikiwa na pointi 4.