Man United kuivaa Liverpool

Manchester,England. Wakati kidonda cha kupoteza kwa mabao 4-3 dhidi ya Chelsea, Alhamisi iliyopita kikiwa hakijapoa, Manchester United leo ina kibarua kingine kigumu nyumbani mbele ya Liverpool kuanzia saa 11:30 jioni.

Ni ushindi tu ambao unaweza kupoza machungu ya mashabiki wa Manchester United lakini knyume na hapo mashabiki wa Liverpool watakuwa wakitamani kupata ushindi ili waendeleze kile walichokifanya ugenini katika mchezo uliopita dhidi ya Sheffield United walipoibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Tofauti na mechi iliyopita ambayo ilikuwa inakutanisha timu mbili ambazo zote hazina matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu, mchezo wa kesho unaihusisha moja inayowaza kutwaa ubingwa na nyingine ambayo sasa inasaka fursa ya kumaliza katika nafasi nne za juu ili ipate nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wenyeji Manchester United wanaingia katika mechi hiyo wakiwa hadi sasa wamekusanya idadi ya pointi 48 katika ligi kuu msimu huu huku Liverpool yenyewe imekusanya pointi 70, kila moja ikiwa imecheza mechi 30.

Kwa Manchester United, ushindi utaweka hai matumaini yao ya kutinga Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na kwa Liverpool, kupata pointi tatu ugenini leo kutaifanya izidi kuchanja mbuga kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.

Ni mchezo unaoipa fursa nzuri Liverpool kulipa kisasi kwa Manchester United cha kutolewa katika mashindano ya Kombe la FA, Machi 17 ilipofungwa mabao 4-3 na ikumbukwe katika mechi ya kwanza baina yao kwenye Ligi Kuu, timu hizo zilitoka sare tasa.

Wageni Liverpool wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na muendelezo wa kufanya vizuri kwenye EPL katika siku za hivi karibuni na kudhihirisha hilo, tangu ilipopoteza dhidi ya Arsenal, Februari 4, imecheza mechi saba mfululizo bila kupoteza ikishinda sita na kutoka sare moja.

Hali ni tofauti kwa wenyeji Manchester United ambao wamekuwa katika hali ngumu kutokana na mwenendo wa kupoteza pointi ambao wamekuwa nao hivi sasa ambapo katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu England, imepata ushindi mara moja tu, kutoka sare moja na kupoteza michezo mitatu.

Namba zinaongea

Historia inaonyesha kuwa Manchester United ni mbabe wa Liverpool pindi zikutanapo kwenye EPL ambapo katika mechi 63 zilizopita baina yao, Man United imeibuka na ushindi mara 29 huku Liverpool ikishinda michezo 19 na zimetoka sare mara 13.

Lakini katika siku za hivi karibuni, Liverpool imekuwa haina unyonge mbele ya Manchester United na kuthibitisha hilo, katika mechi tano zilizopita baina yao za EPL, Liverpool imeibuka na ushindi mara tatu, Man United ikishinda moja na mchezo mmoja ukimalizika kwa sare.

Kumekuwa na angalau mabao matatu ambayo yamekuwa yakifungwa katika mchezo mmoja pindi Man United na Liverpool zilipokutana katika mechi tano zilizopita ambazo Man United walikuwa nyumbani.

Manchester United imekuwa ikiruhusu angalau bao moja katika mechi zake sita nyumbani zilizopita dhidi ya Liverpool ambayo nayo imekuwa ikifunga angalau boja katika kipindi cha kwanza katika mechi zake sita zilizopita.

Mohamed Salah anabakia kuwa tegemeo kubwa la Liverpool katika mchezo wa leo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu na kupiga pasi za mwisho huku kwa Manchester United akiwa ni Bruno Fernandes.

Salah amehusika na idadi ya mabao 25 ya Liverpool msimu huu, akifunga mabao 16 na kupiga pasi za mwisho tisa wakati Fernandes yeye amehusika na idadi ya mabao 13, akifunga mabao matano na kupiga pasi za mwisho sita.

Marefa hawa hapa

Refa Anthony Taylor ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Gary Beswick na Adam Nunn wkaati refa wa akiba akiwa ni Craig Pawson.

Katika teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR), kutakuwa na John Brooks na Richard West.

Chelsea, Spurs ni mtafuano

Kwenye Uwanja wa Bramall Lane, Chelsea ambayo imetoka kutimiza idadi ya mechi sita mfululizo bila kupoteza kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu itakuwa ugenini kukabiliana na Brentford.

Ushindi katika mechi hiyo utaweka hai matumaini yake ya kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Ulaya wakati kwa Brentford utazidi kuongeza faraja katika vita yao ya kuwania kubaki Ligi Kuu.

Jijini London, Tottenham Hotspur itakuw mwenyeji wa Nottingham Forest

Kwingineko hakujapoa

Kutakuwa na mechi tano za Ligi Kuu ya Italia 'Serie A' leo ambapo inayosubiriwa kwa hamu ni ile baina ya Juventus dhidi ya Fiorentina na mechi nyingine itakuwa ni kati ya Frosinone dhidi ya Bologna.

Cagliari itaumana na Atalanta, Monza itaikaribisha Napoli huku Verona ikicheza na Genoa.

Mechi mbili zitachezwa katika Ligi Kuu ya Ujerumani ambapo moja itakuwa baina ya Hoffenheim dhidi ya Augsburg na nyingine itazikutanisha Wolfsburg dhidi ya Borussia Monchengladbach.