Mashindano ya Kimataifa ni fursa iliyokosa uratibu wa Kitaifa
Katibu wa Sekretarieti ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), Paul Bilabaye akizungumza na wadau wa sekta ya utalii jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Hali hii inatajwa kuwa kikwazo kwa taifa kuvuna mapato kutoka kwa watalii wa kibiashara, wageni wa mikutano ya kimataifa na mashindano ya michezo.
Dar es Salaam. Mashindano ya kimataifa kama CHAN na AFCON yameelezwa kuwa ni maeneo ya dhahabu kwa nchi kama Tanzania, ikiwa tu yatachukuliwa kama sehemu ya ajenda ya maendeleo badala ya kuwa matukio ya michezo pekee.
Licha ya kuwa na vivutio vya asili, hoteli bora na miundombinu inayokua kwa kasi, wataalamu wanasema Tanzania bado haijaweka mifumo thabiti ya kitaasisi ya kuongoza sekta hiyo.
Hali hii inatajwa kuwa kikwazo kwa taifa kuvuna mapato kutoka kwa watalii wa kibiashara, wageni wa mikutano ya kimataifa na mashindano ya michezo.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 6, 2025 na Katibu wa Sekretarieti ya Mashindano ya CHAN, Paul Bilabaye ambaye amesema nchi nyingi hupata mapato makubwa kutokana na mnyororo wa huduma unaotengenezwa na matukio hayo kuanzia malazi, usafiri, chakula, burudani, biashara ndogondogo hadi ajira za muda mfupi.
“CHAN siyo mechi tu, ni jukwaa la kiuchumi watu wanakuja kutoka nchi mbalimbali wanakula, wanalala, wanatembelea miji. Hii ni fursa kwa sekta ya utalii, kwa wajasiriamali na kwa nchi kupata mapato ya ndani. Lakini tunaipoteza kwa sababu hatujajipanga kitaasisi,” amesema Bilabaye.
Bilabaye aliweka wazi kuwa licha ya maandalizi mazuri ya michezo, bado kuna mianya inayosababisha picha mbaya kwa wageni na hasara kwa nchi.
“Nilishiriki kuwapokea wageni waliowasili saa sita usiku, walifika kwenye hoteli lakini wahudumu wakasema hawana taarifa. Wageni walikaa na mabegi yao hadi asubuhi. Hii ni picha mbaya kwa taifa na ni mfano mdogo wa fursa zinazopotea,” amesema.
Pia, Bilabaye alitoa mfano wa mji wa Dodoma, unaozalisha zabibu mara mbili kwa mwaka, amesema kipindi cha mashindano kama CHAN kingeweza kutumika pia kuandaa tamasha la zabibu (grape festival) na hivyo kuvutia wageni, kuonyesha bidhaa za ndani, na kukuza ajira kwa vijana.
“Michezo inaweza kuwa kichocheo cha utalii wa ndani tunaweza kuwaandalia wageni wetu burudani za kiutamaduni, chakula cha asili, maonesho ya kilimo na biashara. Hii si kazi ya Wizara ya Michezo pekee, ni ajenda ya taifa,” alisema.
Bilabaye amesema mashindano ya kimataifa hayapaswi kuachwa mikononi mwa mashirikisho ya michezo peke yake, bali yaunganishwe na mipango ya kitaifa ya maendeleo na sekta nyingine kama utalii, miundombinu, utangazaji na uwekezaji.
“Tulipokuwa tunaandika nyaraka za BID ya kuomba uenyeji wa AFCON 2027 kwa Afrika Mashariki, tuliweka viwanja vya Arusha na Azam Complex. Lengo lilikuwa kuunganisha utalii na michezo tukifanikiwa, tutaleta maelfu ya wageni. Lakini hilo haliwezekani bila mfumo rasmi wa kushirikiana,” amesema Bilabaye.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ernest Mwamaja amesema Serikali tayari imetambua kuwa MICE ni zao mahususi la kimkakati katika utalii wa kisasa, na ndio maana limeingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 kama moja ya maeneo ya kipaumbele.
“Hili si suala la ndoto binafsi za wadau ni agizo rasmi la Ilani ya Uchaguzi, Serikali imedhamiria kulikuza na sasa kazi kubwa ni kuimarisha miundombinu, kuunganisha wadau na hatimaye kuanzisha Convention Bureau ya taifa,” amesema Mwamaja.
Amesema pamoja na mafanikio kwenye utalii wa vivutio vya asili, bado Tanzania inaweza kupata mapato makubwa kupitia mikusanyiko mikubwa ya kimataifa, hasa kwa kuunganisha sekta ya michezo, chakula, burudani na usafiri.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Popular Link, Mariam Ndambagenda amesema Tanzania inayo rasilimali ya kuwa kitovu cha mikutano ya kimataifa barani Afrika, lakini inakosa uratibu wa kitaifa.
Ametoa wito kwa Serikali kuanzisha chombo rasmi cha uratibu wa sekta ya MICE ili kuhakikisha wadau wote wananufaika ipasavyo.
“Tunafanya MICE bila kuwa na mfumo, wageni wanakuja kwa mikutano, wanakula, wanalala, lakini hatuwezi kufuatilia faida yake kwa taifa. Hii sekta ina fedha nyingi, mtu anayekuja kwenye mkutano au micheo ana hela,” amesema Ndambagenda.
Amesema sekta hiyo duniani ina thamani ya zaidi ya dola trilioni 3 kwa mwaka, lakini Tanzania bado haijaweka mazingira rafiki ya kuingia rasmi kwenye ushindani wa kimataifa.