Mayele: Ubingwa tayari, bado kiatu tu

Mayele: Taji tayari, bado kiatu tu

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele amesema malengo yake kwenye Ligi Kuu Bara yalikuwa mawili kuhakikisha Yanga inachukua taji baada ya kulikosa kwa misimu minne kisha kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, lakini kubwa kwa sasa ni kiatu cha dhahabu.

Mayele alisema msimu uliopita akiwa Ligi Kuu ya DR Congo alifunga mabao 14 na mara alipotua Yanga alijiwekea nia ya kufikia idadi hiyo na anashukuru ameyavuka akiwa na Yanga amefunga 16, kitu kinachomfanya sasa afikirie zaidi ikiwezekana anyakue tuzo ya mfungaji Bora.

Alisema Yanga tayari imefikia malengo ya kutwaa ubingwa taji muhimu la ubingwa wa ligi walilolikosa kwa misimu minne na kilichobaki wakati huu ni kufikisha malengo yake.

“Malengo yangu ya kwanza kufunga mabao 14, nimeyafikia na kilichobaki mbele yangu ni kuwa mfungaji bora na kuchukua tuzo hii ambayo niweke wazi nataka kweli,” alisema Mayele na kuongeza;

“Ushindani katika kuwania tuzo hii kati yangu na George Mpole au wachezaji wengine ni mkubwa kwani nao wapo imara na bora katika kutimiza majukumu yao ya kufunga mabao,”

“Kuna nyakati nilikutana na wakati mgumu kushindwa kufunga mfululizo kwenye mechi zaidi ya tatu ilikuwa ni presha kubwa kwangu ingawa nilituliza akili na kuamini nitavuka katika kipindi hicho na kweli nilifanikiwa.

“Unajua tayari nimewazoesha mashabiki wa Yanga kutetema kila siku nikifunga kwa maana hiyo ikipita michezo mingi bila ya kufanya hivyo si jambo zuri kwangu na timu kwa ujumla.”

Katika hatua nyingine Mayele alisema tafsiri ya aina yake ya kushangilia wakati anapiga mkono maana yake muda wa kufunga umefika na ile ya kutingisha mabega ameongeza tu kama mbwembwe.

Mayele alisema msimu huu si rahisi kwani ulikuwa wa kwanza kwake ila alikutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa timu zote walizokutana nazo ingawa Yanga ilikuwa bora zaidi hadi kuchukua ubingwa.

Alisema kwenye kikosi cha Yanga kuna wachezaji bora kuanzia wale wanaopata nafasi ya kucheza hata wanatokea benchi kila mmoja amepambana hadi kufikia malengo ya kutwaa taji hilo.

“Baada ya kusherehekea ubingwa huu tumebakiwa na kazi ngumu moja mbele ya kuhakikisha tunapambana na kushinda fainali ya kombe la Shirikisho (ASFC) na naimani kubwa hili tunaliweza,” alisema Mayele kinara wa mabao kwenye ligi akiwa na 16.

Msimu uliopita mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara alikuwa nahodha wa Simba, John Bocco aliyeweka kambani mabao 16, ambayo tayari msimu huu Mayele ameyafikia huku akiwa na michezo mitatu mkononi.