Miquissone aizamisha Al Ahly Dar

Simba hawashikiki, yaichapa Al Ahly

Muktasari:

  • Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi wa soka barani Afrika umeifanya Simba kukamata usukani wa Kundi A, ikiwa imekusanya pointi zote sita katika mechi mbili za kwanza baada ya kuilaza As Vita ya Congo pia kwa bao 1-0.


Mshambuliaji hatari wa Simba, Luis Miqquisone leo ameipa timu yake ushindi mzuri wa nyumbani dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya Misri baada ya kutundika bao pekee katika dakika ya 30 ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa.


Miquisone, ambaye anatumia zaidi mguu wa kushoto, alipata mpira nje kidogo ya eneo la penati. Alipotafuta nafasi ili apige kwa mguu wa kushoto, alikuta ukuta na hapo ndipo akageuka na kuachia kiki kali ya mguu wa kulia iliyompita kipa nyota barani Afrika, Mohamed El Shenawy na kugonga mtambaa panya kabla ya kujaa wavuni.


Bao hilo linaifanya Simba ikamate uongozi wa Kundi A, ikiwa imekusanya pointi zote sita katika mechi mbili baada ya kuishinda AS Vita kwa bao 1-0 ugenini katika mechi ya kwanza.


Ahly, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara tisa, inashika nafasi ya pili sawa na Vita, ambayo jana iliichakaza El Mireikh ya Sudan kwa mabao 4-1 ugenini. Vita na Ahly zina pointi tatu wakati vigogo hao wa Sudan hawana pointi baada ya kufungwa mabao 3-0 na Ahly katika mechi ya kwanza jijini Cairo.


Kocha Didier Gomez alifanya badiliko moja tu katika kikosi kilichoanza dhidi ya Vita, akimuanzishia benchi kiungo Rally Bwalya huku Hassan Dilunga akicheza badala yake upande wa kushoto.


Gomez pia alianza na Chris Mugalu kama mshambuliaji pekee, akimuweka benchi Meddie Kagere, huku nahodha John Bocco akiendelea kuuguza majeraha.


Hata hivyo, alikuwa ni Miquissone aliyeisumbua Ahly, akizungumza uwanja mzima kuasaidia kuokoa na kupeleka mashambulizi, na haikuwa ajabu alipozawadiwa kwa bao hilo safi baada ya kugeuka kwa kasi na kupiga shuti hilo kali kufunga bao lililodumu hadi mwisho.


Ahly, ambayo imetoka kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ilikofungwa na Bayern Munich katika mechi ya nusu fainali, haikuonekana kuchanganyikiwa baada ya kufungwa bao hilo.


Iliendelea kucheza taratibu, wachezaji wakipasiana kana kwamba hawakuwa wanataka kwenda golini, hata hivyo walipokuwa wakikaribia lango la Simba walipiga pasi za haraka haraka ambazo ziliifungua ngome ya Simba iliyoongozwa na Joash Onyango.


Iliongeza kasi dakika kumi za mwisho ilipoonekana kutafuta kwa bidii bao la kusawazisha, lakini utulivu wa mabeki wa Simba na kutopoteza ovyo mipira kulisababisha vigogo hao wa Cairo kutopeleka mashambulizi mfululizo na hivyo kuruhusu kipigo hicho cha kwanza.