Msuva asajiliwa Wydad kwa Sh1.5 bilioni

Muktasari:

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amesajiliwa na miamba ya soka nchini Morocco, Wydad Casablanca kwa kitita cha Sh1.5 bilioni.Msuva asajiliwa Wydad kwa Sh1.5 bilioni

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amesajiliwa na miamba ya soka nchini Morocco, Wydad Casablanca kwa kitita cha Sh1.5 bilioni.

Si tetesi tena kama ambavyo awali, Msuva mwenye miaka 27, amejiunga na miamba hiyo ya soka la Morocco kwa kusaini mkataba wa miaka minne kwa Euro 575, 000.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, inaelezwa kuwa dili la Msuva kujiunga na Wydad lilikamilika tangu Juni na kilichokuwa kikisubiriwa ni kutangazwa kwake kuwa mchezaji rasmi wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ (2019).

Inaelezwa kuwa Wydad ilikuwa ikivutiwa na Msuva tangu 2018, ambao walitwaa Batola Pro na walichokuwa wakipishana ilikuwa ni ada ya uhamisho, lakini mwenyekiti wa Difaa, Abdelatif Moktarid naye hakuwa na mpango wa kumwachia nyota huyo wa zamani wa Yanga.

Msimu huo, Msuva alikuwa moto wa kuotea mbali, akiifungia Difaa El Jadida mabao 13 kwenye ligi na kuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wakiwania kiatu cha ufungaji bora cha msimu huo, alimaliza nyuma ya Mouhcine Lajour wa Raja Casablanca aliyekuwa na mabao 19.

Akizungumzia uhamisho huo, Msuva, ambaye yupo Tunisia na Taifa Stars, alisema ni hatua nyingine kwake katika maisha yake ya soka, amepata nafasi ambayo hakuitegemea kutokana na ukubwa wa klabu hiyo nchini humo.

“Difaa ni klabu ndogo kwa Morocco, nilipambana kuhakikisha napiga hatua, nikijipa uvumilivu huku nikiwa na matumaini kuwa ipo siku nitapiga hatua, ninafuraha kujiunga na Wydad naamini nitapambana kwa kutoa mchango wangu ili kuhakikisha heshima ya klabu inarejea msimu ujao,” alisema Msuva aliyesajiliwa na Difaa akitokea Yanga.