Mukoko afichua ishu yake Yanga

Kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe akiwa katika mazoezi.

BAADA ya tetesi za kiungo wa Yanga, Tonombe Mukoko wa Yanga kudaiwa kugomea mkataba mpya wa klabu ya Yanga, wadau wengi wa timu hiyo walimwona kama anafanya usaliti.

Mwanaspoti lilipiga stori na Mukoko baada ya kumwibukia mazoezini katikati ya wiki naye alisema suala hilo lilivyo akiweka wazi hajawahi kugomea mkataba mpya wa Yanga.

Mukoko alisema hajagomea mkataba mpya, lakini bado hajafuatwa na uongozi wa Yanga ili kujadili juu ya kuongeza ili aendelee kusalia klabuni hapo.

“Sijagoma kuongeza mkataba mpya, ila ukweli hadi sasa sijafuatwa juu ya kuongeza, ila mjue mi bado ni mchezaji wa Yanga kwani nina mkataba uliosaliwa na miezi sita,” alisema Mukoko.

Mukoko alisema suala la kuongeza mkataba litakuwa na kipaumbele kikubwa cha yeye kucheza kwa sababu hilo ndio jambo kubwa anatarajia kuliona ili aendelee kuwepo kwenye timu ya Taifa.

Akizungumzia kuhusu kuhusishwa kuwa yupo mbioni kujiunga na RS Berkane pamoja na Simba, Mukoko alisema; “Hapana! Mi bado ni mchezaji wa Yanga hizo ni tetesi tu kama zingine.”

Mazoezini hapo ilimshuhudia pia kiungo huyu akifanya kikao kizito na Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msola kilichochukua takribani dakika 10.

Mukoko kwenye msimu uliopita alikuwa ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Yanga katika eneo la kiungo akicheza sambamba na Feisal Salum ambaye sasa anacheza kama mshambuliaji wa pili (Namba 10).

Msimu huu Mukoko hapati nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza baada ya kusajiliwa Khalid Aucho na Yanick Bangala ambao wameonyesha pacha nzuri tangu waanze kucheza.

Imeandikwa na Thomas Ng’itu, Olipa Assa na Charity James.