Nkane ang’oa mtu Yanga

Nkane ang’oa mtu Yanga

JUZI Mwanaspoti liliwajulisha kuwa, winga Denis Nkane kutoka Biashara United alikuwa akihesabu saa tu kutambulishwa Jangwani na kweli usiku wa juzi Yanga ilimtambulisha akiwa mmoja ya nyota wapya watatu waliosajiliwa kwenye dirisha dogo.

Wengine waliotua sambamba na Nkane ni kipa Abuutwalib Mshery kutoka Mtibwa Sugar na kiungo fundi wa mpira kutoka Azam, Salum Abukabar ‘Sure Boy’, lakini sasa imefahamika ujio wa winga huyo unamng’oa mtu ndani ya kikosi cha Kocha Nasreddine Nabi.

Nkane amesajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na nusu na kocha Nabi amefichua ujio wake unamlazimisha kuchana mkataba wa winga mwingine aliyepo kikosini kwa sasa ili kutoa nafasi kwake kuliamsha Jangwani kwa raha zake.

Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema ujio wa Nkane ndani ya kikosi chake una maana kubwa na kwamba sasa atakuwa na upana katika kuchagua winga yupi amtumie katika mechi zipi iwe katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) au michuano yoyote watakayoshiriki.

Hata hivyo, Nabi aliweka wazi kwamba kutua kwa Nkane kutaifanya timu yake kuwa na jumla ya mawinga watano na hivyo kumlazimisha kumpunguza mmoja ili kikos chake kiwe na uwiano mzuri kwa kila idara.

“Nkane ni mchezaji ambaye amethibitisha ubora wake akiwa na Biashara United nimemfuatilia tangu nifike hapa Tanzania, anajua kupambana na ana kasi nzuri,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tuna mashindano mengi ambayo kuna wakati unacheza katika viwanja vibovu, huyu ni mchezaji mdogo ambaye amethibitisha anaweza kupambana katika mazingira magumu na hata yale mazuri ni ingizo zuri napenda sana kufanya kazi na vijana.”

Kocha Nabi aliongeza kwa kufafanua; “Kwa sasa tutakuwa na jumla ya mawinga watano, naangalia uwezekano wa kumtoa mmoja ili timu iwe na uwiano mzuri tubaki na wanne, kazi hiyo nitakuja kuifanya nikirejea mapumzikoni.”

Wawinga waliopo sasa kikosini na mmoja lazima apitiwe na panga la Nabi ni pamoja na Deus Kaseke, Dickson Ambundo aliyetua msimu huu kutoka Dodoma Jiji, Farid Mussa na Jesus Moloko aliyesajiliwa pia msimu huu akitokea DR Congo na akiwa ameshafunga mabao matatu.

Nyota hao wamekuwa wakipishana uwanjani katika mechi mbalimbali, huku Moloko akiwa kati ya wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza sambamba na Farid Mussa, huku Ambundo aliingia Yanga na bahati mbaya ya kupata majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.

Ambundo kwa sasa amerejea, huku Kaseke aliyekuwa mmoja wa nyota tegemeo wa Yanga msimu uliopita sambamba na Yacouba Songne akipoteza namba na kutumika zaidi akitokea benchi katika mechi za vinara hao wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 29 baada ya mechi 11 za kwanza msimu huu.