Phiri, Mayele weka niweke

SIMBA inatajwa kuwa kwenye mawindo makali kusaka mshambuliaji ambaye atasaidiana na Moses Phiri, lakini hadi sasa imeunda pacha kali ambayo imefunga nusu ya mabao iliyofunga hadi sasa huku ikiwapoteza wapinzani wao.

Simba eneo la ushambuliaji inaongozwa na Phiri ambaye ameifungia mabao 10 na kutoa aisti moja, huku kiungo mshambuliaji Clatous Chama akifunga mabao mawili na asisti saba.

Wana Msimbazi ndio timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi mzunguko huu Ligi Kuu Bara ukiwa unaelekea mzunguko wa pili, ambapo wamefunga mabao 31, ikiwa ni mabao sita zaidi ya timu inayofuatia. Yanga iliyofunga 25.

Simba wamefunga mabao katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza ambapo kati ya hayo Phiri na Chama ndio wamehusika kwenye upachikaji wa mabao mengi zaidi.

Wawili hao wanafikia nusu ya mabao yaliyofungwa na timu nzima msimu uliopita wakiingia kambani mara 41, ambao kinara alikuwa ni Kibu Denis ambaye aliingia kambani mara nane.

Wakati wawili hao wakiwa mwiba kwa timu pinzani kutokana na wanavyotupia, upande wa Yanga kuna Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao wamehusika na mabao 18 kati ya 25 ya timu hiyo kwenye mechi 14.

Mayele amefunga mabao 10 na kutoa asisti moja sawa na Phiri, huku Fei Toto akifunga mabao matano na asisti mbili na kufanya jumla ya mabao 18 wakiachwa nyuma mabao mawili na pacha ya Simba inayoundwa na Chama na Phiri.

Mastaa hao wanne wa Simba na Yanga ndiyo wanaonekana kuzibeba timu zao - ni Phiri pekee amecheza mechi zote 15 mzunguko wa kwanza akiitumikia timu yake kwa dakika 1275.

Wakati Chama ambaye pia anakipiga Simba amecheza mechi 12 akitumika kwa dakika 1057 na kukosekana mechi tatu kati ya 15 za mzunguko wa kwanza - tatu akikosekana kutokana na adhabu ya kufungiwa na Bodi ya Ligi kutokana na kushindwa kusalimiana na wachezaji wenzake kwenye mechi ya dabi dhidi ya Yanga.

Wakati Mayele ameitumikia Yanga mechi 12 akicheza dakika 897 amekosekana mbili dhidi ya Tanzania Prisons na KMC na bado wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya Namungo.

Fei Toto amecheza dakika 802 kwenye mechi 12 akikosekana michezo miwili kutokana na adhabu ya kadi za njano dhidi ya Ihefu FC timu yake ikikubali kichapo cha bao 1-0 na Mbeya City pale ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0 na wana mchezo mmoja wa kiporo kukamilisha mechi 15 za mzunguko wa kwanza.


WASIKIE WADAU

Akiwazungumzia mastaa hao, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema Simba ina safu nzuri ya ushambuliaji, lakini inatakiwa kuongezewa nguvu kutokana na waliopo kushindwa kutoa changamoto.

“Chama na Phiri ni wazuri na wameonyesha mchango mkubwa ndani ya timu, lakini endapo mmoja wapo akikosekana kunakuwa na changamoto. Hii ni kutokana na waliopo benchi wameshindwa kuonyesha ubora wao,” alisema.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema mzunguko wa kwanza timu zote mbili zimeonyesha ubora eneo la ushambuliaji kutokana na kuwa na wachezaji wenye jicho la kuona goli lakini hawana mbadala wanapokosekana.

“Phiri na Mayele wamethibitisha ubora kila mmoja ameona, lakini viongozi wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanawaongezea nguvu ili waendeleze ubora wao na wasivimbe vichwa kwa kuamini bila wao timu haiwezi kufanya kitu,” alisema.