TFF: Safari yetu ina vituo tusisinzie

Hakuna mtu makini kama msafiri japo wengi pia humwita kafiri. Huyu uhakikisha kuwa kituo anachoshuka amekipatia, hapati usingizi na wala akili haiwazi kingine isipokuwa kituo chake cha mwisho. Kwenye maisha pia tuna safari, ndoto na malengo ni vituo mbalimbali ambavyo tumepanga kupitia ili tufike mahala fulani ambapo tumekuwa tunahitaji kwa kipindi chote hicho cha mapambano.

Soka letu nalo limekuwa na safari, safari ambayo sio wengi waliyoifurahia, safari iliyokuwa na misukosuko mingi lakini walau vituo vyahivi karibuni vimekuwa kwenye miji iliyoendelea. Kwenye ngazi ya klabu Simba ilifika hatua ya robo fainali na kama Taifa tukanufaika kwa kupata uwakilishi wa klabu nne msimu huu. Timu ya Taifa iliibuka kutoka kweye handaki lenye giza kwa miaka thelathini na tisa na hatimaye tukauona mwanga ndani ya Misri kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika.

Ikiwa ni mwanga unaovutia kwenye mboni ya kila mpenda soka, hatuhitaji giza lirejee tukiwa hatuna mbinu za kuwasiliana na kutazamana wakati ukifika. Mipango sahihi ndilo jambo pekee ambalo mpaka sasa kama Taifa tunahitaji na pia ndio wakati ambao historia ya kitaifa kwenye soka inaweza kuweka muhuri wa moto wenye majina ya Karia, Kidau na akina Nyamlani.

Hakuna wakati wenye hamasa kama huu, hakuna kipindi chenye harufu ya fedha za Watanzania kama hiki na pia huu ndio wakati ambao kama Taifa lugha yetu ya Kiswahili kwenye soka letu ina misamiati inayokaribiana kwa kiasi kikubwa.

Tumeshuhudia kocha akiondoka, sawa lakini ni nini kinafuata baada ya hapo? Kituo chetu kinachofuata ni kipi na tunatumia usafiri upi?

Kuanzia ushirikishwaji wa taasisi mbalimbali, wadau mpaka namna ambayo mipango ya kuanzia chini kwa maana ya ligi za mikoa, daraja la kwanza mpaka ligi kuu inabidi ikae kwenye utekelezaji wa kisasa na ambao umejaa uwazi kwa kiasi kikubwa. Usafiri mnaochukua naomba muhakikishe unaweza kubeba mpaka Ligi Daraja la Kwanza, huku kumeoza na watu wanakula vinavyonuka na ladha yake wameshaizoea na wala haiwapi shida kabisa.

Tatizo ni kuwa wanapokuja na tabia ya kuzoea ulaji wa mizoga, wanaambukiza hii tabia kwenye Ligi Kuu na hivyo ubora wa ujumla unakuwa unakosekana kutokana na mazoea mabaya. Kama tumekwama kwenye kuitengeneza chapa ya daraja ya kwanza basi tutatangaze tenda kwa watu wenye mipango mkakati na masoko ili mfanye nao biashara ya kununua mawazo bora, naamini wapo.

Nimefurahi kusikia kuwa kutakuwa na wadhamini wawili wanakuja kwenye Ligi Kuu, safi ndugu zangu. Ingewezekana kabisa kama daraja la kwanza pia mngeiweka kama sehemu ya “package” iwapo kama inashindikana kuuzika kivyake pia. Lakini pia tujifunze namna ya kuwapa wadhamini thamani inayofaa na kuwaweka katika nafasi ya kufurahia wao kuwa wazazi wa ligi hii na waweze kuwahudumia watoto wao katika namna bora zaidi.

Jina la Ettiene Ndiyaragije lilikuwa ni jambo jingine bora lilioibuka kwenye pitia pitia zangu wakati nikiwa naelekea mwishoni mwa andiko hili na sikusita kuliweka kuwa sehemu ya mawazo yangu. TFF wamemchagua kuwa kocha anayekaimu nafasi iliyoachwa wazi na Emmanuel Amunike.

Kuna jambo zuri kwenye mikono ya utendaji wake, anaifahamu ligi yetu vyema. Ameishi kwenye bajeti ndogo na kufahamu namna ya kupata kilichokuwa bora kwa wachezaji na kufanya vyema. Anafahamu shida za wachezaji wa timu ndogo ambazo nyingi zina vijana wengi na pengine inawezekana tukawa tumebahatika kupata Poulsen aliyekaa katika sura ya Ettiene. Inawezekana kabisa akawa ni mtu atakayepuliza hewa ya maisha mapya kwenye soka letu kutokana na falsafa zake.

Bahati nzuri pia ni kuwa jopo alilolichagua linaendana na hiki ninachokiwaza. Selemani Matola alifanya vyema na Simba B kabla hajatua na kuendeleza vipaji vya akina Miraji Athumani, lakini pia mtu kama Juma Mgunda ni aina ya watu ambao wanapumua vyema soka letu.

Ukitazama kwa mbali utaona kuna sura ya moja ya wachezaji ambao walifanya vyema siku za karibuni, Nadir Haroub akiwa meneja wa timu. Huyu anawafahamu wachezaji na anazungumza nao lugha moja ya ujana na ujanja.

Tupo kwenye usafiri ni muhimu kutokulala kwa sababu tukizubaa tu, tutakosa vituo muhimu vya safari yetu kwenye soka.

Hiki ni kipindi chema, kipindi cha kuanza taratibu kuishi katika ulimwengu wa mipango, kipindi cha kufanya majaribio ya sayansi ya mpira, kipindi ambacho TFF inatakiwa kuishi kwenye uhalisia. Tumuunge mkono Ettiene, tuweke mazingira rafiki ya ligi, tuhakikishe klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zinapata hamasa sahihi na kisha tuhakikishe chapa ya ligi yetu inaendelea kukomaa.