Zoran aingilia ishu ya Dejan Simba

STRAIKA Mzungu aliyekuwa akikipiga Simba, Dejan Georgijevic ameshasepa zake alfajiri ya juzi kurudi Serbia, huku Kocha wa zamani wa timu hiyo aliyepo Al Ittihad ya Misri, Zoran Maki akiingilia kati, akisuka mipango ya kumvuta katika klabu anayoinoa sasa.

 Dejan alitangaza kujiuengua Simba kwa madai klabu hiyo imevunja baadhi ya vipengele vya mkataba wake wa miaka mitatu na alikwama kuondoka tangu Jumatano kutokana na kushindwa kumalizana na mabosi ikiwamo kupewa barua ya kumuacha awe mchezaji huru.

Hata hivyo, tayari Dejan kwa sasa anazungumza akiwa kwao, baada ya kupatiwa barua hiyo na anaweza kujiunga na timu yoyote na tayari inadaiwa Kocha Zoran ameanza mipango ya kumbeba aungane naye nchini Misri.

Mwanaspoti limepenyezewa taarifa, Dejan aliyeitumikia Simba kwa siku 52 tu tangu asajiliwe alikubali kuondoka baada ya kupewa barua huku ikielezwa wameafikiana kwa baadhi ya mambo juu ya mkataba huo, ingawa haijawaekwa wazi kwani hakuna kiongozi wa Simba aliyepatika na kufunguka.

Awali kulikuwa na tishio kwa pande hizo mbili kufikishana FIFA, Simba ikisema Dejan ndiye aliyevunja mkataba, ilihali Mzungu naye akilalamika mabosi wa klabu hiyo ndio waliozingua na kumfanya aamue kutoa taarifa mtandaoni na kuondoka kambini visiwani Zanzibar Simba ilipoweka kambi ya muda na kucheza mechi mbili za kirafiki.


ZORAN SASA

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuna mawasiliano ya karibu kati ya Dejan na Kocha Zoran aliyeitumikia timu hiyo kwa siku 67 kabla ya kutimkia Al Ittihad ya Misri.

Mara baada ya Zoran kujulishwa na Dejan kwamba wametibuana, fasta alianza mchakato wa kuwashawishi mabosi wa Al Ittihad kuona namna gani kama wataweza kumsajili kabla ya msimu mpya kuanza nchini humo.

Kwa namna wawili hao walivyo karibu kutokana na uraia wao, halitakuwa jambo la kushangaza muda wowote kuanzia sasa kusikia Dejan akitangazwa kuwa mchezaji mpya wa Al Ittihad kwani wamekuwa wakiwasiliana kila hatua ya mgogoro wake na Simba ulivyoku ukiendelea. Zoran amekuwa akivutiwa na Dejan ndio maana alikubali usajili wake katika kikosi cha Simba na alikuwa akimtumia mara kwa mara ingawa baada ya kuondoka mambo yalikuwa tofauti kwa mchezaji huyo, licha ya mara kadhaa viongozi wa Simba kusema wao ndio waliopendekeza asajiliwe.

Zoran kutokana na kuvutiwa na uchezaji wa Dejan ndio maana amewashawishi mabosi zake wa Al Ittihad kumchukua straika huyo na kama mambo yatakwenda vizuri kabla ya msimu ujao kuanza atatambulishwa kama nyota mpya.

Mwanaspoti lilimtafuta Zoran alisema Dejan ni miongoni mwa washambuliaji wazuri wenye uwezo wa kufunga ila kuna changamoto zilimfanya kushindwa kuanza vizuri katika kikosi cha Simba.

“Dejan hakuwepo katika maandalizi ya msimu (Pre-season), alicheza Tanzania kwa mara ya kwanza, vitu vingi vilikuwa vigeni kwake na mambo mengine ya msingi yalikuwa changamoto kwa upande wake,” alisema Zoran na kuongeza;

“Niliamini kama angeweza kukaa kwa muda ndani ya kikosi cha Simba na kuzoea mazingira angekuwa msaada kwa timu kwani anaweza kufunga kutokana na aina yake uchezaji ila hakuna namna tena baada ya kuamua kuondoka,”

“Hakuna anayefahamu kesho yake, hivyo kwa Dejan halitakuwa jambo la kushangaza kumuona akijiunga na Al Ittihad kwani ni miongoni mwa washambuliaji wazuri wanaoweza kutimiza majukumu yake. Kwa nini isiwezekane kuja kucheza hapa kama usajili wake ukikamilika,” alisema Zoran.


MGUNDA KIROHO SAFI

Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema hadi sasa roho yake iko kwatu kutokana na namna kikosi kinavyoimarika kadri siku zinavyosidi kusonga mbele akiwa na timu hiyo iliyomchukua kutoka Coastal Union.

Mgunda ambaye usiku wa jana aliiongoza Simba katika mechi ya pili ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji kabla maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primiero de Agosto Alhamisi hii kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza Jumapili ijayo.

“Kuna mabadiliko makubwa na wachezaji wameanza kumeza falsafa zangu na tunaamini mambo yatakuwa bora kadri tunavyozidi kupambana, mwanzoni ilikuwa ngumu wachezaji walikuwa wageni, ila sasa kila kitu kipo freshi,” alisema Mgunda aliyeiongoza timu hiyo katika mechi tatu kabla ya jana na kushinda zote bila kuruhusu bao lolote, mbali na mechi mbili za kirafiki za Zanzibar ikishinda pia zote.