Achana na Mbappe, kuna siri za mastaa wapya Real Madrid

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo mpya aliyejiunga na timu hiyo akitokea PSG, juzi aliduwazwa baada ya kukabidhiwa chumba maalumu chenye hadhi ya nyota tano, ambacho atakitumia kwa ajili ya kupumzika na shughuli nyingine akiwa klabuni hapo

Madrid, Hispania, Habari kali ya wiki hii ni kitendo cha mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe kupewa chumba chake maalumu kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo.

Mshambuliaji huyo mpya aliyejiunga na timu hiyo akitokea PSG, juzi aliduwazwa baada ya kukabidhiwa chumba maalumu chenye hadhi ya nyota tano, ambacho atakitumia kwa ajili ya kupumzika na shughuli nyingine akiwa klabuni hapo.

Inaelezwa kuwa eneo hilo lilijengwa kwa zaidi ya Pauni 100 milioni na chumba cha staa huyo ndicho chenye gharama kubwa zaidi kikiwa na hadhi ya nyota tano.

Real Madrid imekuwa na kawaida ya kugawa vyumba vyenye hadhi ya juu kwa mastaa wake katika eneo hilo la mazoezi la Valdebebas Park, ambapo kila mchezaji anakuwa kwenye chumba chake binafsi, ambapo hata milango inafunguka kwa alama za vidole za mchezaji husika.

Hata hivyo, Mbappe siyo pekee ambaye amekutana sapraizi kwenye timu hiyo, inaonekana kuwa ni mtindo wa maisha ya Madrid ambapo kila mchezaji mkubwa anapotua kwenye timu hiyo anakuwa na kitu chake spesho, vingine vimebaki kuwa siri.


Cristiano Ronaldo (maegesho)

Cristiano Ronaldo alijiunga na Real Madrid akitokea Manchester United mwaka 2009, akiwa mchezaji mwenye heshima kubwa kutokana na kiwango chake alichokuwa akikionyesha uwanjani baada ya kuwa ameshatwaa makombe yote makubwa.

Alipotua Madrid alifanikiwa kutwaa makombe mawili ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne, pamoja na heshima nyingine ambayo Ronaldo alikuwa akipewa kwenye timu hiyo, yeye siku ya kwanza mazoezini alikuta ana eneo maalumu la kuengesha gari lake ikiwa na kibao chenye jina lake na alilitumia hadi siku alipoondoka.


Iker Casillas (mpokea funguo)

Iker Casillas alikuwa kipa mwenye mafanikio makubwa akiwa na Real Madrid, lakini alipewa heshima kubwa kwa kuwa alikuwa mtoto wa nyumbani.

Ndiyo klabu pekee aliyoichezea kwa mafanikio makubwa akiwa alifanikiwa kutwaa ubingwa wa La Liga mara tano na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu.

Kipa huyo aliyeichezea timu hiyo michezo 911, siku moja baada ya kupewa unahodha alifika mazoezini na kumkuta mtu maalumu ambaye alikuwa akimpokea funguo za gari lake na kuzipeleka sehemu maalumu, lakini alikuwa akitoka mazoezini anamkuta yule jamaa anamsubiri na kumkabidhi funguo zake. 

Siku anaondoka Madrid hakuna kiongozi yoyote ambaye alihudhuria mkutano wake wa kuaga, akaangua kilio.


David Beckham (jezi)

Huyu ni kiungo wa zamani wa Manchester ambaye alikuwa maarufu sana akiwa na jezi namba saba na kuna wakati ilikuwa inaonekana kama vile ni nembo yake ya maisha.

Lakini wakati anajiunga na Madrid mwaka 2003 alikuta mkali wa timu hiyo, Raul Gonzalez ndiye anavaa jezi hiyo, akiwa ana heshima kubwa baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa mara tatu.

Anasema kwenye kitabu chake, alielewa hofu iliyokuwepo kwenye timu hiyo kwa ajili ya jezi namba saba, alipoulizwa kuhusu jezi anayotaka, akawaambia mabosi wa Real Madrid, wamweleze zilizopo akatajiwa jezi namba 23, akaichukua na kuivaa kwa kuwa alikuwa anampenda mcheza kikapu Jordan.

Baada ya hapo alipokwenda kwenye vyumba siku ya mechi ya kwanza ya Real, alikuta amewekewa jezi nne tofauti za Jordan zimetundikwa zikiwa na namba 23, baada ya kuzitoa ndiyo akaikuta jezi yake.


Guti (alamu)

Ni mashabiki wachache sana wanamkumbuka staa huyu aliyekuwa Real Madrid ambaye alifanya mambo makubwa lakini akawa haheshimiwi.

Guti ambaye alikaa Real Madrid kwa misimu 15, alitwaa Ligi ya Mabingwa mara tatu na La Liga mara tano, hakuwahi kupewa heshima inayotakiwa kwenye timu hiyo.

Mwaka 2009, siku chache baada ya Madrid kumuajiri kocha mpya Manuel Pellegrini staa huyo alichelewa mazoezini kwa saa mbili hali ambayo iliwashtua watu wengi.

Baada ya kuulizwa nini kilitokea, alijibu kuwa, aliweka alamu kwenye saa yake ikachelewa kuita, kutokana na ukongwe wake kwenye timu hiyo alisamehewa, lakini kesho yake klabu ilimkabidhi saa mpya ya thamani yenye alamu ya sauti ya juu ili asichelewa tena.


Zinedine Zidane (namba 5)

Staa na kocha kwa sasa Zinedine Zidane alijiunga na Real Madrid akitokea Juventus mwaka 2001, akiwa ameshakuwa staa mkubwa.

Aliwashangaza wengi baada ya kucheza mchezo wa kwanza akiwa amevaa jezi namba tano badala ya 21 aliyokuwa anavaa Juventus.

Anasema alipofika, Rais wa Madrid Florentino Perez, alimweleza kuwa hapendi mchezaji anayevaa jezi namba 25, 30, 35. 

Alisema bosi huyo alimwambia, namba moja ni kwa ajili ya kipa, yeye achague nyingine yoyote mwisho namba 10, atampa.

Anasema alimuuliza bosi huyo ni namba gani haina mtu, akamjibu (Manolo) Sanchis ameondoka na alikuwa anavaa jezi namba tano, Zidane akasema anaitaka hiyohiyo ambayo haina mtu.
Anasema jezi hiyo ndiyo ilifungua urafiki wake na Perez hadi leo wanakunywa chai pamoja.