Mbappe atua Madrid kibosi

Muktasari:

  • Real Madrid imethibitisha kumsajili Kylian Mbappe kwa mkata wa miaka mitano hadi 2029.

Madrid. Baada ya maswali mengi, anaenda wapi, Uarabuni, England au Hispania. Hatimaye mabingwa wa Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga, Real Madrid wametoa majibu hayo kwa kuthibitisha kukamilisha dili la Kylian Mbappe kutoka Paris Saint Germain ya Ufaransa.

Taarifa hiyo imechapishwa leo Jumatatu Juni 3,2024, katika kurasa rasmi za Madrid ambao pia ni mabingwa wa Klabu Bingwa Barani Ulaya.

Mshambuliaji huyo ataitumikia Madrid kwa mkataba wa miaka mitano ambapo utakamilika 2029.

Mbappe (25) aliigharimu PSG pauni milioni 166 mwaka 2018 lakini anaondoka bila malipo baada ya mkataba wake kumalizika.

Nahodha huyo wa Ufaransa amesaini mkataba wa miaka mitano na Real Madrid wenye thamani ya Euro 12.8 milioni kwa mwaka baada ya kodi, ambapo atapokea bonasi ya kusaini zaidi ya Euro 85 milioni kutoka kwa Madrid kwa kipindi tofauti ndani ya huo mkataba wake.

Endapo PSG ingemuuza staa huyo ingejipatia karibu Pauni 220 milioni (Euro 187.5 milioni) ya gharama ya jumla.

"Ndoto imetimia. Nina furaha sana na ninajivunia kujiunga na klabu ya ndoto yangu ya Real Madrid.

Hakuna anayeweza kuelewa jinsi nilivyo na furaha hivi sasa."

"Siwezi kusubiri kukuona, Madridistas, na asante kwa usaidizi wako wa ajabu." Amesema Mbappe.

Sakata la staa huyo kutua Madrid lilianza muda mrefu ambapo ilifika hatua ya kuigomea PSG hadi Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alipoingilia kati na kumbakisha nchini humo.

Mbappe ndio mfungaji wa muda wote wa PSG akifunga mabao 256 katika mechi 308 alizocheza tangu ajiunge na miamba hito ya Ufaransa akitokea AS Monaco.

Pia, staa huyo amewahi kuwa mchezaji bora wa msimu mara tatu katika Ligi ya Ufaransa 2018, 2019 na 2022.