Mbappe anaacha mabilioni haya PSG

Muktasari:

  • Mbappe alisajiliwa na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco kwa ada ya uhamisho kiasi cha Euro 180 milioni na kufanya awe mchezaji wa pili ghali duniani nyuma ya Neymar ambaye PSG ilimnunua kwa ada ya Euro 222 milioni kutoka Barcelona.

Paris. Uamuzi wa Kylian Mbappe kuachana na PSG ili ajiunge na Real Madrid (kwa mujibu wa tetesi) utamfanya nyota huyo kuyakosa mabilioni ya fedha ambayo angevuna kama angeamua kubakia kwa mabingwa hao wa Ufaransa.

 Jana Mbappe alitangaza rasmi kuwa ataachana na PSG mara baada ya kumalizika kwa msimu huu na licha ya kutosema wapi ataelekea, habari kutoka vyanzo mbalimbali vya uhakika zinaripoti kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameshafikia makubaliano ya kujiunga na Real Madrid.

"Ni ngumu, ngumu sana. Sikuwahi kufikiria kama itakuwa ngumu kiasi hiki kutoa hili tangazo.

"Kuondoka kwenye nchi yangu, Ufaransa, Ligue 1, mashindano ninayoyafahamu. Lakini, nadhani nahitaji hii kitu, changamoto mpy baada ya miaka saba," alisema Mbappe.

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho Mbappe atakikosa kwa kuamua kuachana na PSG ni katika mshahara kwani amelazimika kukubali kulipwa kiasi mshahara pungufu usiofikia hata nusu ya ule ambao amekuwa akiupata kwenye klabu aliyopo kwa sasa ili ajiunge na Real Madrid.

Akiwa na PSG, mchezaji huyo anapata kiasi cha Euro 75 milioni (Sh 209 bilioni) lakini ndani ya Real Madrid, mshambuliaji huyo atalipwa kiasi kinachotajwa kuwa Euro 15 milioni (Sh 41 bilioni) na amelazimika kukubali kupunguza kiwango cha mshahara ili kuiwezesha Real Madrid kutovunja sheria ya matumizi ya fedha iliyowekwa katika Ligi Kuu ya Hispania.

Mshambuliaji huyo pia anakiacha kiasi cha Euro 90 milioni (Sh251 bilioni) ambacho angepewa kama bonasi ya kubakia ndani ya PSG kwa msimu wa 2024/2025.

Hata hivyo pamoja na kupokea mshahara huo kiduchu ndani ya Real Madrid kulinganisha na ule anaoupata akiwa na PSG, Mbappe anatarajiwa kuvuna kiasi cha Euro 150 milioni (Sh 419 bilioni) ambacho ni dau lake la kujiunga na miamba hiyo ya Hispania.

Lakini pia ndani ya Real Madrid, mchezaji huyo atakuwa na umiliki mkubwa wa haki za matumizi ya taswira yake pamoja na mikataba binafsi.

Mbappe (25) ameitumikia PSG kwa miaka saba na ambapo amecheza mechi 306 na kufunga mabao 255 na kutoa pasi 108 za mabao katika misimu sita.

Ameshinda mataji sita ya ligi na Kombe la Ufaransa mara tatu tangu alipotua mwaka 2018, lakini ameshindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pia, amekuwa mchezaji bora wa msimu mara tano na kuwa mfungaji bora mara 10 katika ligi ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Mbappe ana utajiri unaokadiriwa kufikia kiasi cha Dola 120 milioni (Sh 311 bilioni).