Adebayor ajisogeza Simba, apania kimataifa

STAA wa Berkane ya Morocco, Victorien Adebayor wa RS Berkane ya Morocco ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa bado akili yake ni kuchezea Simba haswa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiungo huyo mshambuliaji, alionyesha kiwango kikubwa akiwa na USGN ya Niger iliyocheza na Simba kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. USGN Jijini Dar es Salaam walilala mabao 4-0 na nyumbani wakatoka sare ya bao 1-1.
Alianza kuwindwa na Simba na Yanga lakini gharama yake ikawakimbiza ndipo Berkane chini ya Florent Ibenge ikamwaga mpunga na kumnyama lakini amejikuta akikosa namba na sasa anaiota Simba.
Adebayor amewatia mzuka mabosi wa Simba akiwaaambia kuwa inawezekana kama wakijiongeza safari hii akiwa Berkane wanaweza kumpata kwa wepesi kama Yanga ilivyomnyaka Tuisila Kisinda.
"Nilitamani kucheza Simba,ni klabu ambayo ilionyesha kila hatua ya kunihitaji, hasa mashabiki wao nakumbuka sana upendo walionionyesha nikiwa hapo Tanzania,"alisema Adebayor ambaye vigogo wa Simba wanamfikiria lakini wamekiri kuhofia kwavile anakosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Berkane.
"Wakati ule kulikuwa na ugumu kwao walitakiwa kukamilisha dili lile kwa klabu mbili kitu ambacho waliona ni kigumu. Bado naikumbuka Simba nawakumbuka sana mashabiki wake,naamini utakuja wakati naweza kuja kuichezea Simba hivikaribuni,"alisema na kuongeza kwamba kama Simba watakuwa siriazi sasa anaweza kutua Msimbazi kufanya yake.
Adebayor alisema amefurahishwa na hatua ya wekundu hao kuendeleza kiwango chao katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na anatamani sana kuwa sehemu ya mafanikio yao.
"Kila mchezaji anapenda kuichezea klabu yenye kiwango kizuri katika mashindano ya Kimataifa,nimefurahishwa na hatua ya kutinga kwao makundi.
"Napenda kiwango cha soka wachezaji wao lakini kikubwa ni mzuka wa mashabiki wao wanapocheza nyumbani inavutia sana kuona hasa wakiwa mashabiki wako,"alisema mchezaji huyo aliyewahi kucheza Ufaransa, Denmark, Ghana na Misri kwa misimu tofauti.