Adhabu ya waliofanya utovu wa nidhamu Yanga yaanikwa
Muktasari:
- Yanga imerejea jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Shinyanga walikoshinda mechi yao dhidi ya Mwadui, lakini kocha Nesreddine Nabi amefunguka kuhusu tatizo la nidhamu kwa wachezaji wake.
YANGA imerejea jijini Dar es Salaam ikitokea mkoani Shinyanga walikoshinda mechi yao dhidi ya Mwadui, lakini kocha Nesreddine Nabi amefunguka kuhusu tatizo la nidhamu kwa wachezaji wake.
Yanga iliwasimamisha wachezaji wake watatu wa kikosi cha kwanza akiwamo nahodha wao mkuu beki Lamine Moro, kipa wao Metacha Mnata na mshambuliaji Michael Sarpong wote wakidaiwa kuwa na utovu wa nidhamu.
Akizungumzia hatua hiyo Nabi ameliambia Mwanaspoti katika mahojiano maalum kuwa hatua alizozichukua kwa wachezaji hao kwa kuwaondoa kikosini ni muendelezo wa kile alichokisema mara tu baada ya kutua nchini.
“Nilisema wakati nafika hapa siku ya kwanza, hakuna mafanikio kama utakuwa huna nidhamu, ni lazima kila mmoja hapa awe na rekodi nzuri ya nidhamu.
“Tumeamua kuwachukulia hatua hii hawa wachezaji ili kuonyesha kile ambacho tunataka kukisimamia hapa na hii itakuwa ni fundisho kwa wengine,” alisema Nabi.
ADHABU YAO HII
Nabi alisema bado wachezaji hao wana nafasi ya kurudi kwenye kikosi chake lakini lazima watakumbana na adhabu ya kukatwa pesa kama faini ya makosa waliyofanya.
Alisema adhabu hiyo itatumika kuwakumbusha wachezaji wengine kutofanya makosa kama hayo wakati mwingine.
“Hawa ni kama watoto katika familia wana nafasi ya kurudi kwenye timu tena na kutumikia klabu yao ila ni lazima kila mmoja alipe pesa ambayo watakatwa katika malipo yao, hakuna atakayeepuka adhabu hiyo.
“Tunahitaji pia kuwafundisha wengine kupitia hawa, wakijirekebisha tutawarudisha waendelee kuitumikia timu kama kawaida,” alisema Nabi.
WASIKIE MABOSI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandisi Hersi Said ameliambia Mwanaspoti kwamba uongozi wao umesikitishwa na makosa ya wachezaji hao na kwamba wanaungana na uamuzi wa kocha wao.
Alisema walijua kuna shida ya nidhamu katika kikosi chao na ndio sababu walimleta kocha huyo ambaye hana masihara katika nidhamu.
Alisema tayari beki wao Lamine amekumbana na rungu la kupigwa faini na wakati wowote atarejea kambini huku Sarpong na Mnata nao wakiandaliwa kupita njia kama hiyo.
“Uongozi hatuungi mkono makosa ya nidhamu na yanasikitisha, tuko pamoja na kocha kwa hatua zote za nidhamu atakazochukua kwa mchezaji yoyote.
“Tumekuwa tukiongea na kocha (Nabi) amekuwa akisisitiza hakuna staa mkubwa katika timu yake kitu muhimu au staa kwake ni klabu tu, uongozi tuko pamoja naye katika kulifanyia kazi hili la nidhamu na hatutamuingilia katika lolote katika uamuzi atakaochukua,” alisema.