Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Alianza Peter Tino sasa Fei Toto

Muktasari:

  • Mwisho wa miaka ya 1970, Tanzania haikuwa taifa lenye heshima kubwa katika soka la Afrika.

Katika safari ndefu ya soka la Tanzania, yapo mabao mengi yaliyofungwa na Taifa Stars lakini katika historia ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), yapo mabao mawili ambayo yamebeba uzito wa aina yake.

Bao la kwanza lilifungwa mwaka 1979 mjini Ndola, Zambia na Peter Tino, huku la pili likifungwa juzi Jumatano siku moja kabla ya kuumaliza mwaka 2025 mjini Rabat, Morocco na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wakati Taifa Stars ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia.

Kati ya mabao hayo mawili kuna tofauti ya miaka 46, iliyojaa subira, maumivu, kukata tamaa na hatimaye matumaini mapya ambapo kwa mara ya kwanza Taifa Stars imetinga hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Huku akijihakikishia kuvuna Dola 800,000 (zaidi ya Sh1.9bilioni) kutoka CAF ikiwa ni fungu la zawadi kwa kutinga hatua hiyo.

BAO LA NDOLA

Mwisho wa miaka ya 1970, Tanzania haikuwa taifa lenye heshima kubwa katika soka la Afrika. Miundombinu ilikuwa duni, maandalizi hayakuwa bora kama ilivyo sasa na Taifa Stars ilitegemea zaidi vipaji vya ndani.

Katika mazingira hayo, Tanzania iliingia kwenye mechi ngumu ya kufuzu AFCON 1980 dhidi ya Zambia, ugenini mjini Ndola. Presha ilikuwa kubwa, wakati Wazambia wakihitaji kuona timu yao ikifanya vizuri katika mechi hiyo kibao kiliwageukia.

Peter Tino aliandika historia. Bao lake halikuwa la kawaida. Lilikuwa bao la kuipeleka Tanzania AFCON kwa mara ya kwanza.

Bao hilo lilimaanisha mengi, lilifungua ukurasa mpya wa historia huku likiwapa, Watanzania imani kuwa wanaweza kushindana Afrika hata kama Tanzania haikufanya vizuri AFCON 1980, uwepo tu katika fainali hizo ulikuwa ushindi wa kihistoria.

MIAKA YA SUBIRA

Baada ya 1980, Tanzania ilipotea katika ramani ya AFCON kwa muda mrefu. Ilirejea baada ya miaka 39 na kushiriki fainali za 2019 kisha 2023 lakini kila awamu iliishia hatua hiyo. Kila kizazi kilikuja na matumaini mapya, lakini matokeo yalibaki yale yale, kuishia hatua ya makundi.

Katika fainali za 2019 ambazo zilifanyika Misri, Tanzania iliburuza mkia katika Kundi C baada ya kufungwa mechi zote tatu za hatua hiyo dhidi ya Senegal kwa mabao 2-0, Kenya 3-2 na Algeria kwa mabao 3-0.

Kwa upande wa fainali za Ivory Coast 2023, Taifa Stars ilimaliza pia mkiani katika kundi F lakini safari hiyo ikikusanya pointi mbili kwa kupoteza mechi moja dhidi ya Morocco kwa mabao 3-0 kisha ikatoa sare dhidi ya Zambia kwa bao 1-1 na DR Congo 0-0.

Kwa zaidi ya miongo minne, Taifa Stars ilikuwa ikisaka bao jingine la kihistoria, bao la kuvuka hatua inayofuata. Watanzania wakasubiri, wakavumilia, wakiamini siku moja historia ingebadilika.

MWIKO ULIVYOVUNJWA RABAT

AFCON 2025 nchini Morocco haikuanza na matarajio makubwa kwa Tanzania. Wengi waliona kikosi cha kocha Miguel Gamondi kimeenda kupata sare moja au mbili, kisha kurejea nyumbani.

Lakini kizazi cha sasa cha Taifa Stars kilikuwa tofauti. Kilikuwa na nidhamu, umoja na imani ya kuweka historia mpya. Katika mechi ya maamuzi dhidi ya Tunisia, Tanzania ilihitaji matokeo chanya ili kujiweka kwenye nafasi ya kufuzu kama moja ya timu bora za tatu.

Hiyo ilikuwa ni baada ya kuanza kwa kupoteza dhidi ya Nigeria kwa mabao 2-1, ikafuata sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda. Ndipo Feisal Salum alipofanya jambo ambalo litabaki kwenye historia.

Bao lake la kusawazisha mjini Rabat halikuwa tu goli la kawaida lilikuwa bao la kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania AFCON.

Katika mechi ya juzi ya kukamilisha hatua ya makundi dhidi ya Tunisia, Fei alikirudia kile alichokifanya Kwa Mkapa mwaka 2020 katika mechi ya makundi ya kuwania fainali za AFCON kwa kufunga bao lililoipa Stars sate ya 1-1 baada ya awali Tanzania kulala ugenini bao 1-0.

Kikosi cha Stars kilicheza kwa nidhamu kubwa licha ya kosa la beki wa kati, Ibrahim Bacca lililozaa penalti baada ya VAR kumng’amua faulo aliyofanya liitanguliza Tunisia na kuonekana kama safari ya Stars imeishia hapo kabla ya sekunde chache baada ya kuanza kipindi cha kwanza Fei kuifunga bao hilo muhimu lililioivunja Tanzania.

Tanzania imefuzu kama mshindwa bora ikiipiku Angola ambao wamelingana nao uwiano wa mabao ikiwa ni -1, lakini tofauti na mabao ya kufunga na kufingwa imewabeba Stars iliyofunga mabao matatu na kufungwa manne wakati wapinzani wao wakiwa na mabao mawili na kufungwa matatu.

Katika mechi hiyo kocha Miguel Gamondi alifanya mabadiliko machache tofauti na kikosi kilichotoka sare ya 1-1 na Uganda kwa kumpumzisha Zuberi Foba na kumsimamisha Hussein Masalanga langoni, huku Dickson Job akianza sambamba na Ibrahim Bacca na Bakar Mwamnyeto na nahodha Mbwana Samatta akichukua nafasi ya Kelvin John na timu kuonekana kuwa na uwiano mzuri na kuibana Tunisia iliyokuwa ikihitaji sare tu iingie 16 Bora.

MAANA MBILI KUBWA

Bao la Peter Tino (1979) lilikuwa bao la kuingia. Lilikuwa la kufungua mlango wa Afrika, la kuonyesha kuwa Tanzania inaweza kuwepo katika michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.

Bao la Feisal (2025) lilikuwa bao la kuthibitisha ukuaji. Lilikuwa la kuvuka mipaka, la kuondoa mkosi wa miaka 46, la kuonyesha kuwa Tanzania sasa inaweza kushindana, si kushiriki tu.

MOROCCO TENA

Baada ya bao la Feisal, Tanzania sasa inakutana na Morocco, wenyeji wa fainali hizi, katika hatua ya 16 bora.

Akizungumza kuhusu kazi kubwa iliyopo mbele yao, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, anasisitiza kuwa ni wakati wa kuendelea kuamini, kujiandaa kwa umakini na kuthubutu zaidi:

“Hakuna ambacho kinashindikana kwenye soka. Kila kitu kinaanza pale wachezaji wanapojitahidi kwenye mazoezi, wakitengeneza umoja na kujiandaa kwa kila mechi. Tumeandika historia hadi sasa na sasa ni wakati wetu kuionyesha kuwa Taifa Stars ipo tayari kwa changamoto yoyote,” alisema.