Alves ndani ya gereza na makombe 43
Muktasari:
- Alves staa mwenye mafanikio makubwa ya kisoka duniani baada ya kutwaa makombe makubwa 43, akiwa na timu ya taifa na klabu alizopita, alifanya tukio hilo Desemba 30, 2022 kwenye klabu ya usiku.
Barcelona, Hispania. Staa wa zamani wa Barcelona, Dani Alves, amekutwa na hatia ya kufanya unyanyasaji wa kijinsia kwa msichana mdogo, jijini Barcelona, Hispania na kuhukumiwa kwenda jela miaka minne na nusu.
Alves staa mwenye mafanikio makubwa ya kisoka duniani baada ya kutwaa makombe makubwa 43, akiwa na timu ya taifa na klabu alizopita, alifanya tukio hilo Desemba 30, 2022 kwenye klabu ya usiku akiwa amelewa chakari.
Mbali na kifungo hicho, mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye amezaliwa kwenye Mji wa Juazeiro, Brazil anatakiwa kulipa faini ya Pauni 130,000 sawa na Sh400 milioni, kwa mwathirika huyo.
Awali Alves, mwenye watoto wawili alipinga kuhusika na kesi hiyo huku akieleza hamfahamu mwanamke huyo, lakini baadaye alibadilisha maneno yake na kusema ni kweli alikutana naye lakini kwa makubaliano maalumu.
Awali taarifa ilisema Alves anayetajwa kuwa beki bora zaidi wa pembeni duniani, aligoma kusema ukweli kwa kuwa alihofia kuachwa na mke wake ambaye alionekana kukasirishwa na mashtaka hayo.
Mmoja kati ya mashahidi waliokuwepo mahakamani alikuwa ni mke wake wa zamani Joana Sanz, ambaye aliiambia mahakama siku ya tukio, Alves alirudi nyumbani akiwa ananuk pombe na alijigonga kwenye viti kabla ya kulala kitandani na hakumuuliza jambo lolote.
Baada ya hukumu hiyo beki huyo alijaribu kuomba nafasi ya kukata rufaa lakini majaji walikataa kwa kinachoelezwa wamejiridhisha ni kweli alifanya unyanyasaji huo na amekuwa akibadilisha maelezo yake kila siku.
Baadhi ya ushahidi uliotolewa unasema msichana huyo alishindwa kujitetea kwa kuwa beki huyo mwenye nguvu alimkandamiza kwa magoti ukutani.
Alves ambaye anatajwa kuwa na fedha nyingi, alisitishiwa mkataba na klabu ya Mexico UNAM Pumas, baada ya kukamatwa Hispania alipokwenda kuhudhuria mazishi ya mama mkwe wake mwaka jana.
Staa huyo ambaye pia alikuwa anaweza kucheza kama winga ameitumikia Brazil kwenye michezo 126 na kufunga mabao manane, katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kuichezea timu hiyo kwenye mashindano makubwa.
Beki huyo aliyeanza kufundishwa soka na baba yake, ana uwezo mkubwa wa kupiga krosi na faulo na alipata mafanikio makubwa akiwa na Barcelona, ambayo aliichezea michezo 391 na kufunga mabao 21.
Pia alizitumikia timu kubwa za Sevilla, Juventus, Paris Saint-Germain na Sao Paulo ambako ameacha historia ya kucheza jumla ya michezo 910, akifunga mabao 67 kwenye timu nane alizozichea hadi sasa huku akikusanya kitita kikubwa cha fedha.
Hazina ya makombe
Alves ni mmoja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa zaidi kwenye upande wa makombe akiwa ameshatwaa kwenye kila ligi aliyocheza.
Akiwa na Barcelona alitwaa makombe manane ya La Liga, Copa del Rey mara nne,
Supercopa de España mara nne, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, UEFA Super Cup mara tatu na klabu Bingwa Dunia mara tatu.
Alves ambaye alienda PSG akionekana ni sehemu ambayo atamalizia soka lake, alitwaa Ligue 1 mara mbili, huku akiwa na Juventus akitwaa Serie A mara moja akiwa na tuzo binafsi zaidi ya 40.
Kesi nyingine:
Novemba 16, 2023, Alves alikutwa na hatia ya kukwepa kodi Hispania kutoka na fedha alizolipwa kwenye haki ya picha zake kuanzia msimu wa 2009–10 na 2010–11 na alipigwa faini ya Pauni 3.2 milioni, zaidi ya Sh9 bilioni.