Amorim ashangazwa na kiwango cha United

Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amesema anashangazwa na kiwango cha timu yake baada ya kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England ambao United ilionyesha kiwango bora.
Liverpool ilitoka nyuma baada ya Lisandro Martinez kufunga bao la kuongoza kwa United kabla ya Cody Gakpo na Mohamed Salah kuipatia Liverpool mabao mawili, lakini Amad Diallo alisawazisha dakika ya 80, na kuipa United pointi moja akitokea benchi.
Baada ya mchezo kumalizika kocha wa United, Ruben Amorim amesema ameshangazwa na upambanaji wa timu yake kwenye mechi nyingine kuwa tofauti kama walivyofanya Anfield.
"Ni vigumu kuelewa jinsi tulivyoweza kucheza hivi leo halafu kushindwa kuendeleza kiwango hichi kwenye mechi nyingine. Sidhani kama ni suala la mfumo au mbinu, tulikuwa na mazungumzo baada ya kushinda dhidi ya Manchester City, lakini bado hali ilijirudia kwenye mechi zilizofuata, tunahitaji kuwa na kiwango bora zaidi,” amesema Amorim.
Naye naodha wa United, Bruno Fernandez alikubaliana na kauli ya kocha wake, akisema: "Tumekosolewa mara nyingi kwa sababu matokeo yetu hayaridhishi, hata leo, hatuwezi kufurahia sare kwa sababu tunahitaji pointi zaidi kuliko wapinzani wetu, kama tumeweza kucheza hivi dhidi ya Liverpool ambayo ni timu bora msimu huu, ni kwanini tusifanye hivi kwa kila timu?"
Bao alilofunga Mohamed Salah linamfanya ahusike katika mabao 31 akiwa amefunga 18 na kutoa pasi za mwisho 13 katika mechi 19 alizocheza msimu huu kwenye Ligi Kuu England. Machester United inashindwa kupata ushindi baada ya kucheza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu ikifungwa tatu na kutoa sare moja wakati Liverpool ikiwa haijapoteza mechi 15 mfululizo tangu Septemba 14, 2024 ilipofungwa na Nottingham Forest, bao 1-0 kwenye uwanja wa Anfield.
Liverpool inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 46 ikifuatiwa na Arsenal nafasi ya pili yenye pointi 40, Nottingham Forest inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 huku Chelsea ikiwa ya nne na pointi 36 wakati Manchester United bado inajitafuta ikiwa nafasi ya 13 na pointi 23.