Angola yaonja ushindi wa kwanza ikiifunga Zambia CHAN 2024
Muktasari:
- Tanzania ndiyo ambayo imeshafuzu kucheza hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi tatu mfululizo katika kundi B.
Timu ya Taifa ya Angola imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza kwenye mashindano ya CHAN 2024 baada ya kuichapa Zambia kwa mabao 2-1.
Katika mchezo huo wa kundi A uliochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi imeshuhudiwa Angola ikitoka nyuma na kuibuka na ushindi huo baada ya kutanguliwa na Zambia.
Bao la Zambia limefungwa na kiungo, Dominic Chanda katika dakika ya 73 kabla ya Kaporal kuisawazishia Angola katika dakika ya 79 kisha kufunga tena bao la ushindi dakika ya 86.
Baada ya kuibuka na ushindi huo Angola inasogea hadi nafasi ya pili kwenye kundi A ikifikisha pointi nne katika mechi tatu ilizocheza nyuma ya wenyeji Kenya ambao wanaongoza kundi wakiwa na pointi saba.
Morocco ambao wamepoteza leo dhidi ya Kenya wameshuka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili sawa na DR. Congo wanaoshika nafasi ya tatu.
Zambia wanaonekana wadhaifu kwenye kundi A kwani ndiyo wanaobuluza mkia baada ya kupoteza mechi mbili walizocheza dhidi ya DR. Congo na leo dhidi ya Angola.
Kwa matokeo haya bado hakuna timu iliyojihakikishia kufuzu hatua ya mtoano ambapo zinasubiliwa mechi za mwisho kuamua atakayesonga katika hatua ya robo fainali.
Hadi sasa ni Tanzania pekee ndiyo ambayo imeshafuzu kucheza hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi tatu mfululizo katika kundi B.