Arsenal, Madrid zaanza kutamba Ulaya
Muktasari:
- Licha ya kuwakosa mastaa wake muhimu akiwemo nahodha Martin Odegaard, Bukayo Saka na William Saliba kikosi cha Mikel Arteta kilionyesha ubora wa kikosi kipana.
Arsenal imeanza kwa kishindo mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Athletic Bilbao, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa San Mamés, Bilbao, Hispania.
Licha ya kuwakosa mastaa wake muhimu akiwemo nahodha Martin Odegaard, Bukayo Saka na William Saliba kutokana na majeraha, kikosi cha Mikel Arteta kilionyesha ubora wa kikosi kipana kilichojengwa kwa bajeti ya pauni milioni 250.
Bao la kwanza liliwekwa kimiani dakika ya 72 na Gabriel Martinelli, aliyefunga sekunde 36 tu baada ya kuingia akitokea benchi, akimalizia kazi nzuri ya Leandro Trossard.
Dakika 15 baadaye wawili hao walibadilishana majukumu, safari hii Martinelli akipiga pasi ya bao kwa Trossard aliyefunga la pili na kuzima matumaini ya wenyeji.
Athletic Bilbao walionekana kuanza kwa kasi kupitia Inaki Williams na Oihan Sancet waliokuwa wakisumbua safu ya ulinzi ya Arsenal. Hata hivyo, juhudi zao zilikwama baada ya Arsenal kuimarika kipindi cha pili na kutumia ubora wa wachezaji waliotoka benchi.
Straika mpya Viktor Gyokeres aliendelea kuonyesha kwamba anakaribia kuwaka moto, licha ya kuvaa bandeji baada ya kugongana vichwa na beki Gabriel. mshambuliaji huyo aliwasumbua mabeki wa Bilbao kwa mbio na nguvu, ingawa alikosa nafasi mbili za wazi.
Mbali na mechi ya Arsenal zipo mechi nyingine ambazo zilichezwa jana kwenye mashindano hayo makubwa Ulaya ambapo ilishuhudiwa Mabingwa wa kihistoria Real Madrid wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Olympique de Marseille ya Ufaransa.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, nyota wa Madrid Kylian Mbappé ndiye alieibuka shujaa wa mechi baada ya kufunga mabao yote mawili kwa mikwaju ya penalti katika dakika ya 22 na 81.
Katika dakika ya 71 Madrid ilipata pigo baada ya naodha wake, Daniel Carvajal kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kwa kichwa golikipa wa Marseille, Gerónimo Rulli.
Matokeo ya mechi nyingine ilishuhudiwa Tottenham ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Villarreal, Benfica ikikubali kipigo cha mabao 3-2 ikiwa nyumbani dhidi ya Qarabag, Royale Union SG nayo iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya PSV wakati Juventus na Dortmund zikitoshana nguvu kwa kutoa sare ya mabao 4-4.
Mechi za leo Ligi ya Mabingwa Ulaya
Olympiacos vs Pafos
Slavia Praha vs Bodø/Glimt
Ajax vs Inter Milan
Bayern München vs Chelsea
Liverpool vs Atlético Madrid
Paris Saint-Germain vs Atalanta