Arsenal yamalizana na Chelsea kwa Noni Madueke

Muktasari:
- Madueke alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu uliopita, akicheza mechi nyingi ikiwemo fainali ya Europa Conference League.
London, England. Arsenal imefikia makubaliano na Chelsea kuhusu uhamisho wa winga wa England, Noni Madueke, kwa dau la pauni milioni 52 sawa na Shilingi za Kitanzania 166 bilioni na sasa uhamisho huo uko mbioni kukamilika rasmi.

Madueke, mwenye umri wa miaka 23, alifanya mazoezi na wachezaji wenzake wa Chelsea Alhamisi asubuhi jijini New York, wakijiandaa na fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Paris Saint-Germain, lakini kuna uwezekano mdogo sana wa kuhusika kwenye kikosi kitakachocheza Jumapili kutokana na hatua za mwisho za makubaliano na Arsenal.
Taarifa zinasema tayari amekubali masharti binafsi ya mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ya Emirates na hakuna vikwazo vilivyojitokeza kwenye mazungumzo ya kibinafsi na upande wa Chelsea.
Madueke alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Chelsea msimu uliopita, akicheza mechi nyingi ikiwemo fainali ya Europa Conference League ambayo walishinda dhidi ya Real Betis. Pia alitumika katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Fluminense kama mchezaji wa akiba.

Arsenal, chini ya kocha Mikel Arteta, imekuwa ikisaka mshambuliaji wa pembeni katika dirisha hili la usajili, huku Madueke akitajwa kuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye orodha ya juu. Licha ya kuwa walikuwa wakitafuta winga wa upande wa kushoto.
Winga huyo wa zamani wa PSV Eindhoven ni mguu wa kushoto na hupendelea kucheza upande wa kulia nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Bukayo Saka katika kikosi cha Arsenal lakini pia ameonyesha uwezo wa kucheza upande wa kushoto na kufanya hivyo mara kadhaa akiwa na Chelsea.
Endapo uhamisho huo utakamilika, Madueke atakuwa mchezaji wa tatu kujiunga na Arsenal kutoka Chelsea katika dirisha hili la usajili, baada ya mlinda mlango Kepa Arrizabalaga aliyesajiliwa kwa pauni milioni 5 (Sh16 bilioni).

Kwa upande wa Chelsea, ujio wa kinda mwenye kipaji, Estevao Willian (18) kutoka Palmeiras, unaonekana kuchukua nafasi ya Madueke. Estevao tayari alionyesha uwezo wake kwa kufunga bao kali dhidi ya Chelsea katika mechi ya Klabu Bingwa Dunia.

Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, ameonekana kuwa tayari kumuacha Madueke aondoke, akisema: "Ujumbe wangu kwa wachezaji na kwa klabu ni kwamba nataka wale tu wanaofurahia kuwa nasi. Wale wasio na furaha, wako huru kuondoka. Noni amekuwa mchezaji muhimu msimu huu."
Iwapo dili hilo litakamilika, Arsenal itakuwa imeongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji na kuleta ushindani kwa nyota kama Gabriel Martinelli kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya England.