Arsenal yamtibulia Amorim United, Liverpool hoi
Muktasari:
- Amorim alimkosa beki wake wa kati Lisandro Martinez lakini nafasi yake ilichukuliwa na mlinzi mtata Noussair Mazraoui.
London, England. Arsenal imeendeleza ubabe mbele ya Manchester United baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 jana kwenye Uwanja wa Emirates.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Jurrien Timber dakika ya 54, kabla ya William Saliba kufunga bao lingine dakika ya 73. Baada ya ushindi wa jana Arsenal inaifunga Man United kwa mara ya nne mfululizo kwenye Ligi Kuu England ‘EPL’.
Arsenal imepata mabao mengi kwa mipira ya kona kuliko timu yoyote kwenye Ligi kuu ikiwa imefunga mabao 20 tangu msimu wa 2023-2024 lakini mengi yakiwa yameweka wavuni na walinzi.
Ruben Amorim amepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi tangu Desemba 2023 alipofungwa mabao 2-3 dhidi ya Guimaraes akiwa kocha wa Sporting CP na tangu alipotua United alikuwa hajapoteza mchezo wowote.
Matokeo hayo yameifanya United kuwa nafasi 11 kwenye msimamo huu ukiwa mchezo wa rekodi kwa Arsenal kwa kuibuka na ushindi kwenye michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kufanya hivyo dhidi ya wapinzani wao.
Huu ulikuwa mmchezo wa 500 kwa Arsenal kucheza kwenye Uwanja wa Emirates tangu ilipoondoka kwenye Uwanja wa Highbury ikiwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi kama itafanya vizuri kwenye michezo ya mwishoni mwa mwaka.
Katika mchezo wa juzi, Arsenal ilikuwa bila beki wake mahiri Gabriel pamoja na Jakub Kiwior, lakini bado waliokuwepo waliweza kufanya kazi yao kwa ubora wa hali ya juu.
Amorim alimkosa beki wake wa kati Lisandro Martinez lakini nafasi yake ilichukuliwa na mlinzi mtata Noussair Mazraoui.
Michezo mingine, iliopigwa jana ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza Manchester City ikipata ushindi wa mabao 3-0 baada ya kupoteza mechi nne mfululizo huku Chelsea ikiifunga Southampton mabao 5-1, Aston Villa ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Brentford, Everton ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wolverhampton wakati Liverpool ikilazimishwa sare ya mabao 3-3 ugenini dhidi ya Newcastle United.
Hii ni sare ya pili kwa Liverpool msimu huu baada ya awali kutoka sare na Arsenal ya mabao 2-2.
Baada ya matokeo ya jana, Liverpool inabaki nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 35, Chelsea imesogea nafasi ya pili ikiwa na idadi kubwa ya mabao 31 ikiizidi Arsenal mabao mawili huku Man City ikisogea nafasi ya nne ikiwa na pointi 26. Iwapo Brighton itashinda mechi ya leo dhidi ya Fulham itaishusha Man City kurudi nafasi ya tano.
Leo itapigwa michezo miwili ya Ligi kuu England ambapo Bournemouth itakuwa nyumbani kuwakaribisha Tottenham Hotspur wakati Brighton itakuwa ugenini dhidi ya Fulham.