Arsenal yathibitisha kumuuza Leandro Trossard Uturuki
Arsenal imetangaza rasmi kufikia makubaliano na Besiktas ya kuwauzia mshambuliaji wake Leandro Trossard.
Licha ya Arsenal kutoweka hadharani dau la kumuuza nyota huyo wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 31, inaripotiwa kwamba uhamisho huo utaifanya ivune kiasi cha Euro 18 milioni (Sh54 bilioni).
Arsenal itapata Euro 2 milioni (Sh6 bilioni) za ziada kutokana na mafanikio ya mchezaji huyo ndani ya Besiktas.
“Tunathibitisha kwamba tumefikia makubaliano na Besiktas kwa uhamisho wa Leandro Trossard.
“Baada ya makubaliano kufikiwa kuhusu ada ya uhamisho, Leo (Trossard) mwenye umri wa miaka 31, ameruhusiwa kusafiri kwenda Istanbul (Uturuki) kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya na kukamilisha taratibu rasmi za kujiunga na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki,” imesema taarifa ya Arsenal.
Trossard anaondoka Arsenal baada ya kuitumikia kwa miaka mitatu na nusu tangu alipojiunga nayo, Januari 2023 akitokea Brighton.
Ameshinda mataji mawili akiwa na Arsenal ambayo ni Kombe la Ligi Kuu England msimu uliomalizika na Ngao ya Jamii mwaka 2023.
Katika msimu uliopita, Trossard alifunga bao pekee la ushindi la Arsenal ugenini dhidi ya West Ham ambalo lilichangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Englanda ambao iliukosa kwa miaka 22.
Katika miaka mitatu na nusu ambayo Trossard ameitumikia Arsenal, amecheza mechi 174 za mashindano tofauti huku akifunga mabao 36 na kupiga pasi 34 za mwisho.