Azam FC, KMC kazi ipo
Muktasari:
Michezo hiyo ya hatua ya 16 bora itachezwa kati ya Februari 22 hadi 25 ili kupatikana timu nane zitakazotinga raundi ya tano ambayo ni robo fainali.
Dar es Salaam. Droo ya kombe la Shirikilisho la Azam Sports Federation (ASFC), imefanyika jana kwa Yanga kupangwa na Majimaji huku Azam dhidi ya KMC ambayo imepanda daraja.
Yanga ambayo ipo kwenye maandalizi ya michuano ya klabu bingwa Afrika, itasafiri kama ilivyokuwa kwenye hatua iliyopita ya kombe hilo kwa kuifuata Majimaji mkoani Songea.
Azam itakuwa ugenini kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex ambao nao pia umekuwa ukitumiwa na KMC katika michezo yake ya nyumbani hivyo KCM itaikaribisha Azam kwenye mchezo huo.
Kocha wa Dodoma FC mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ atarejea mkoani Shinyanga alipokuwa akiifundisha Mwadui kuchuana na Stand United.
JKT Tanzania itacheza na Ndanda FC, Kiluvya United dhidi ya Tanzania Prisons, Singida United itapepetana na Polisi Tanzania, Njombe Mji itaikaribisha Mbao FC, Buseresere dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mara baada ya kupatikana kwa timu hizo, itachezeshwa tena droo ambayo itabainisha timu zitakazo chuana hatua hiyo pamoja na hatua ya nusu fainali.