Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam, Singida BS zasaka heshima CAF

Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Singida Black Stars, leo watakuwa katika viwanja na miji tofauti nje na ndani ya Tanzania katika mechi za raundi ya tatu ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika

Ushindi kwa wawakilishi hao wa Tanzania utaweka hai matumaini yao ya kutinga hatua ya robo fainali.

Azam FC itakuwa kwenye Uwanja wa Nyayo nchini Kenya ambako kuanzia saa 10:00 jioni itacheza na wenyeji wao Nairobi United.

Azam iliyopoteza mechi zote mbili ilizocheza hadi sasa kwenye kundi B, inapaswa kuepuka matokeo ya sare au kupoteza mechi ya leo kwani matokeo hayo yatazidi kuiweka katika uwezekano finyu wa kusonga mbele.

Ikiwa inacheza hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake, ilianza kwa kufungwa mabao 2-0, dhidi ya Maniema Union ya DR Congo, kisha mechi ya pili ikapoteza kwa bao 1-0, mbele ya Wydad Casablanca ya Morocco.

Nairobi United iliyoanzishwa rasmi mwaka 2015, ikifahamika kwa jina la Balaji EPZ kabla ya kubadilishwa mwaka 2022 na kuitwa Nairobi United, inaburuza mkiani mwa kundi hilo, baada ya kuchapwa pia mechi zote mbili ilizocheza hadi sasa msimu huu.

Nairobi United ilianza hatua ya makundi kwa kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, kisha kuchapwa bao 1-0 na Maniema Union ya DR Congo, huku timu zote zikikutana zikiwa safu ya ushambuliaji haijafunga bao lolote hadi sasa.

Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amenukuliwa akisema baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate iliyoisha suluhu (0-0) kuwa ilikuwa ni njia mojawapo ya maandalizi muhimu, ndio maana alifanya mabadiliko pia kwa baadhi ya wachezaji.

Mechi nyingine itakayoanza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar itahusisha Singida Black Stars inayoburuza mkia katika kundi C dhidi ya AS Otoho ya Congo iliyo nafasi ya tatu na pointi zake tatu.

Singida Black Stars inayocheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo, ilianza kwa kuchapwa mabao 2-0 na CR Belouizdad ya Algeria, kisha kutoa sare nyumbani ya bao 1-1, dhidi ya vinara wa kundi, Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Kwa upande wa AS Otoho iliyo nafasi ya pili na pointi tatu, ilianza hatua ya makundi kwa kuchapwa bao 1-0 na vinara wa kundi hilo, Stellenbosch yenye pointi nne, kisha mechi ya pili kuiduwaza CR Belouizdad kwa kuichapa nyumbani mabao 4-1.

Kocha wa Singida Black Stars, Mkenya David Ouma, alisema changamoto kubwa anayopambana nayo katika kikosi hicho ni eneo la ushambuliaji, kwani licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ila utulivu sio mzuri wa kuzibadilisha kuwa mabao.

"Mechi yetu ya mwisho ya Ligi Kuu tuliyopoteza bao 1-0, dhidi ya JKT Tanzania tulitengeneza zaidi ya nafasi tano za wazi kipindi cha kwanza ingawa hatukuzitumia vizuri, mashindano ni tofauti hivyo, tunahitaji kuongeza umakini," alisema Ouma.