Azam yapaa kileleni ikimfunga mbabe wa Yanga

Dar es Salaam. Azam FC imepaa kileleni baada ya kuichapa Ihefu mabao 3-1 katika Uwanja wa Highland Estate jijini Mbeya.

Mabao ya Azam yamefungawa na Feisal Salum dakika ya 34 na mawili yakifungwa kipindi cha pili na Sospeter Bajana huku Ihefu ikiapata bao dakika ya 90 na Jaffar Kabaya.

Katika mchezo huo Azam imeonyesha kiwango bora na kufanikiwa kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Ihefu chini ya kocha wake Moses Basena raia wa Uganda imeendelea kukosa ushindi katika mechi nne alizosimamia tangu atue kikosini humo, Oktoba 16 kuchukua nafasi ya Zuberi Katwila.

Katika michezo minne hiyo, wamepoteza miwili mbele ya Simba 2-1 na dhidi ya Azam na sare mbele ya Coastal Union na Singida Big Stars na kubaki nafasi ya 11 kwa pointi nane baada ya michezo tisa.

Ushindi huo unakuwa wa pili mfululizo ikiendeleza dozi ya mabao matatu baada ya kufanya hivyo katika mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa huko Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Azam inapanda kileleni ikiishusha Yanga licha ya kutangulia mechi mbili na bingwa huyo mtetezi na tatu dhidi ya Simba huku ikisubiri mchezo wa watani hao kujua hatma ya kubaki juu au kushushwa nafasi ya pili.