Aziz Ki alivyomtia aibu Motsepe Loftus

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Lilikuwa pambano la kuvutia likiwa na wachezaji nyota duniani. Hata hivyo, sidhani kama lilikuwa pambano bora kama hili la Ijumaa usiku. Ijumaa usiku lilikuwa pambano la kutetea roho na kuzamisha roho ngumu. Mamelodi Sundowns dhidi ya Yanga.

Achana na Cairo. Tuanzie Loftus, uwanja ambao Julai 2009 nilikuwa kwenye moja kati ya viti vyake nikitazama pambano la michuano ya mabara kati ya Brazil na Italia.

Lilikuwa pambano la kuvutia likiwa na wachezaji nyota duniani. Hata hivyo, sidhani kama lilikuwa pambano bora kama hili la Ijumaa usiku. Ijumaa usiku lilikuwa pambano la kutetea roho na kuzamisha roho ngumu. Mamelodi Sundowns dhidi ya Yanga.

Mamelodi waliingia uwanjani kwa lengo la kuiteketeza roho ngumu ya Yanga waliyokutana nayo Dar es salaam wiki moja iliyopita. Yanga waliingia uwanjani kutetea roho yao kama walivyofanya wiki moja iliyopita.

Manuel Gamondi aliendelea alipoishia, safari hii mbele ya mashabiki wa Mamelodi ambao walikuwa wakiimba kwa nguvu kabla ya mechi na wakati wa mechi. Waafrika Kusini kuimba ni jadi yao. Tangu wakati ule wa zama za ubaguzi wa rangi hadi leo ambapo wamehamishia muziki wao katika amapiano.

Yanga walibana njia zote za Mamelodi. Waliziba njia kwa kupitia wachezaji wao. Maxi Nzengeli akageuka kuwa beki wa kulia. Mudathir Yahya akakichafua katikati. Bakar Mwamnyeto akaosha mipira yote ya juu pamoja na rafiki yake, Ibrahim Bacca. Mbele yao Jonas Mkude akaifanya kazi ya Khalid Aucho.

Lakini kabla ya yote unaweza kumsifu pia kipa Djigui Diarra. Ana ukomavu. Kama mechi za Afcon hazikumshinda angeshindwaje mechi hii ya Mamelodi. Yeye na wachezaji wengi wa Mamelodi walikuwa pamoja kule Ivory Coast katika michuano ya Afcon. Diarra sio kipa tu bali ni kiongozi uwanjani. Alijua muda gani acheleweshe mpira, alijua namna ya kuzitokea krosi na kuzikamata, alijua kupiga mipira mirefu.

Mbele walimuacha Aziz Ki ambaye kiukweli hawakumsogelea vema wakati walipopata mipira ingawa yeye na Joseph Guede walijitahidi kadri walivyoweza kusumbuana na mabeki wa Mamelodi. Asifiwe Guede ambaye alionekana kuwa mzuri wa kukaa na mipira.

Kadri mechi ilivyosogea ndivyo ambavyo Mamelodi walionekana kupoteza mipango. Mashabiki wao walidhani Yanga walikuwa wamebahatisha kwa kile walichokifanya Temeke. Wakati mwamuzi alipopuliza filimbi ya kupeleka wachezaji wote katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya mapumziko mashabiki wa Mamelodi wakajua namna ambavyo pambano la Temeke lilivyokwenda.

Kipindi cha pili kiliendelea pale pale ambapo kipindi cha kwanza kiliishia. Lakini baada ya muda kidogo wachezaji wa Mamelodi wakaonekana kuanza kuishiwa pumzi na pale ndipo Yanga walipoanza kuwa na mchakato mzuri zaidi wa kupeleka mpira mbele walau kusaka bao la ugenini. Kilichokuja baada ya hapo ni historia.

Bao la Aziz Ki ndio kitu kilifuata. Ni katika mashambulizi haya haya ya haraka ambayo Yanga walipeleka mbele langoni mwa Mamelodi. Kennedy Musonda akampasia Aziz Ki aliyeunyanyua mpira vema kabla ya kupiga shuti kali ambalo lilimshinda nguvu kipa wa Mamelodi, Ronwen Williams. Bao. Lilikuwa bao halali. Hakukuwa na suala la kwamba mpira haukuvuka wote. Hapana. Mpira ulivuka wote.

Nini kilifuata? Maongezi kati ya mwamuzi wa kati na watu waliopo chumba cha VAR. Ilichukua dakika nne kuuficha ukweli ambao ulikuwa dhahiri. Kazi chafu ambayo zigo aliangushiwa mwamuzi. Wakati watu wanajadili kwanini mwamuzi hakwenda kujiridhisha kutazama katika kioo chake cha pembeni, binafsi sikuona hata haja ya mwamuzi kwenda kujiridhisha. Lilikuwa bao dhahiri ambalo watu wa VAR walipaswa kumwambia mwamuzi aweke kati.

Kama sio kuhongwa basi ulikuwa ni uamuzi mzito kwao. Katika ardhi ya Afrika Kusini, jijini Pretoria, timu ya Rais wa CAF, Patrick Motsepe. Unawapa vipi Yanga bao katika dakika ya 58? Mamelodi walikuwa wameshindwa kuziona nyavu Dar es salaam kwa dakika 90 na chache za nyongeza. Walikuwa wameshindwa kuziona nyavu katika dakika 58 wakiwa nyumbani Pretoria. Wangewezaje kufunga mabao mawili katika dakika 32 zilizobaki?

Napata hisia kama bao la Aziz lingefungwa dakika za mwanzo mwanzo za kipindi cha kwanza basi huenda waamuzi wa VAR wangeamuru lisimame kwa sababu wangehisi Mamelodi wangekuwa na muda wa kusawazisha na kurudisha. Lakini kwa jinsi mechi ambavyo ilikuwa inakwenda waliona ugumu wa Mamelodi kusonga mbele. Wakaamua walichoamua.

Nilikiwa nimekaa na wachezaji wa Mamelodi ambao hawakuhusika na mechi. Niliwaonyesha video ya bao la Aziz Ki na wote walikubali kwamba lilikuwa bao halali kwa Yanga. Kilichotokea kimekuwa fedheha kubwa kwa soka la Afrika hasa ikizingatiwa kwamba mmiliki wa Mamelodi ni Rais wa CAF lakini pia ni milionea. Itaendelea kuwa fedheha kubwa kwake kwa muda mrefu ujao.

Mitaani nilikotembea mashabiki wengi wa soka Afrika Kusini kuanzia kwa Mamelodi wenyewe hadi Kaizer Chiefs na Orlando Pirates wamesikia fedheha kwa kilichotokea. Wakati mashabiki wa Mamelodi wakiwa wanasikia aibu, mashabiki wa Kaizer na Orlando wamekuwa wakiwazomea na kumshutumu Motsepe kwa kuharibu mpira.

Baada ya hapo pumzi ya Mamelodi iliendelea kukatika na Clement Mzize akakosa bao la wazi ambalo lingeweza kuwavusha Yanga kwenda hatua ya nusu fainali. Mzize lazima afahamu kwamba nafasi zile zinatokea mara chache katika pambano gumu la soka, dhidi ya Mamelodi ugenini.

Anapaswa kuwa makini zaidi. Unaweza kupoteza nafasi ile dhidi ya Coastal Union na mashabiki wakaona kawaida. Hawawezi kuona kawaida ukikosa dhidi ya Mamelodi ugenini katika pambano ambalo linaweza kuipatia Yanga dola milioni moja na nusu. Alifanya sahihi zaidi wakati alipofunga bao la pili dhidi ya Al Merrikh pale Kigali.

Baada ya muda pambano likamalizika zikaja penalti. Yanga hawakuonekana kujiandaa kiakili kukabiliana na penalti. Sijui akili zao ziliwaambia kwamba watapita ndani ya dakika 90? Hawakuonekana kuwa tayari kisaikolojia isipokuwa kwa kipa Diarra ambaye wote tunafahamu uhodari wake. Penalti ya kwanza tu Aziz akamlenga kipa.

Aziz anaonekana hana nguvu ya kiakili katika mechi kama hizi. Anacheza soka kwa sababu analifahamu lakini hapambani sana katika mechi ngumu. Anakuwa mzuri wakati Yanga wanapolielemea lango la adui huku maadui wakiwa wanalinda lango lao. Hapo anaweza kuwa mtatuzi. Lakini kuanzia ndani ya dakika 90 Aziz huwa hakabi na wakati mwingine anapoteza mipira ovyo.

Penalti hii alienda kuipiga kama penalti nyingine tu. Mchezaji wa kwanza wa kupiga penalti anapaswa kuwa makini na kuwafungulia wenzake njia. Sawa, wachezaji wengi mahiri duniani wanakosa penalti lakini Aziz alipaswa kuwa makini zaidi na kumjua kipa aliyekuwa mbele yake ambaye alikuwa naye kuwa Ivory Coast.

Baadaye Diarra akairudisha Yanga mchezoni lakini Dickson Job naye akaenda kupiga penalti ya kitoto. Wao walikuwa makini na penalti zao zilizobakia wakaanza kupiga juu ya Diarra. Hakuna kipa ambaye angeweza kudaka penalti zao. Baadaye Bacca akaenda kutupigia penalti ambayo mpaka leo hatuna uhakika kama mpira umetua ardhini. Yanga nje.

Ndiyo, huo ulikuwa mwisho wa Yanga. Waliondolewa kishujaa katika ardhi ya Motsepe huku sababu ya msingi ya kuondolewa kwao ikijulikana. Mpaka wakati mwingine tena lakini Yanga wameshindana tena katika michuano hii kama walivyofanya katika michuano ya Shirikisho msimu uliopita. Hakuna cha kuwadai sana.

Tunachoweza kuwadai ni kurudi tena katika hatua hizi msimu ujao. Sababu wanayo. Nia yao. Uwezo wanao. Wakirudi na kuzoeazoea kupambana katika hatua hizi wanaweza kufika mbali zaidi. Wana kijana mwenye akili na mipango, Hersi Said. Wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa sababu wameelekeza akili yao katika kufanya vizuri na wamewekeza zaidi katika vitendo. Hadi wakati ujao.