Aziz Ki, Fei Toto warudi tena vitani
Muktasari:
- Aziz Ki na Fei Toto wote wawili wanashindania tuzo za mchezaji bora wa msimu, kiungo bora wa msimu, na mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB katika hafla ya TFF ya 2023/2024, itakayofanyika Dar es Salaam, Agosti 1, 2024.
Dar es Salaam. Ushindani ulioteka hisia za wengi katika Ligi Kuu msimu uliomalizika baina ya viungo Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC umeibuliwa upya kabla ya kuanza kwa msimu ujao baada ya wawili hao kutangazwa kuwekwa katika orodha ya kushindania vipengele vitatu tofauti katika hafla ya tuzo za TFF za msimu wa 2023/2024 itakayofanyika, Dar es Salaam, Agosti Mosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF leo, sherehe za tuzo hizo za msimu wa 2023/2024 zitafanyika Agosti Mosi jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki.
Aziz Ki na Fei Toto majina yao yamejitokeza katika kuwania tuzo kwenye vipengele vya mchezaji bora wa msimu, kiungo bora wa msimu na mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Katika orodha ya wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Fei Toto na Aziz Ki wanashindana na Kipre Junior (Azam), Djigui Diarra (Yanga), Ley Matampi (Coastal Union), Kouassi Yao (Yanga), Ibrahim Hamad (Yanga) na Mohammed Hussein (Simba).
Tuzo ya kiungo bora wa ligi inawaniwa na Fei Toto, Aziz Ki na Kipre Junior.
Kwa upande wa kipengele cha tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB, wanaowania ni Aziz Ki, Clement Mzize, Fei Toto, Ibrahim Bacca na Kipre Junior.
Tuzo ya mchezaji bora wa Tanzania wa kiume anayecheza nje inawaniwa na Mbwana Samatta, Novatus Dismas na Himid Mao wakati tuzo ya mchezaji bora mwanamke anayecheza nje inawaniwa na Aisha Masaka, Clara Luvanga na Opa Clement.
Tuzo ya mchezaji bora wa soka la ufukweni inawaniwa na Jaruph Juma, Yahya Tumbo na Abdillah Mohammed.
Aisha Mnuka, Stumai Abdallah, Kaeda Wilson, Violeth Nicholaus na Vivian Corazone wanawania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya wanawake na tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya wanawake inawaniwa na Juma Mgunda, Esther Chabruma na Noah Kanyonga.
Tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara inawaniwa na Miguel Gamondi, David Ouma na Bruno Ferry wakati Ley Matampi, Ayoub Lakred na Djigui Diarra wanashindania tuzo ya kipa bora wa ligi kuu.
Kiujumla idadi ya tuzo 62 za vipengele tofauti zitawaniwa katika hafla hiyo ambapo zipo zitakazoshindaniwa na wachezaji mmoja mmoja, timu, makocha, maofisa wengine wa mpira wa miguu, marefa na wadau wa soka.