Baba Msuva afunguka dili la Yanga
Muktasari:
- Mzazi huyo ambaye ni msimamizi wa staa huyo wa zamani wa Yanga, amekiri kusikia mwanae akihusishwa na Yanga lakini anachojua kwa sasa akili yake haipo Tanzania.
BABA mzazi wa winga wa Taifa Stars, Happy God Msuva ameliambia Mwanaspoti dili la Simon Msuva si tu haliwezekani Yanga bali kwa klabu yoyote ya Tanzania.
Mzazi huyo ambaye ni msimamizi wa staa huyo wa zamani wa Yanga, amekiri kusikia mwanae akihusishwa na Yanga lakini anachojua kwa sasa akili yake haipo Tanzania.
Tunajua Yanga wanasaka saini ya mmoja kati ya Msuva, Mkongomani Macabi Lilepo na George Mpole wa FC Lupopo.
Amesema habari zinazoendelea bado haziendani na malengo makubwa ya mwanae kuendelea kukipiga nje ya nchi na muda wowote kuanza sasa dili likitiki anatimka.“Mwanangu ananiambia, baba bado nataka kucheza nje ikitokea kucheza hapa nyumbani labda baadae lakini kwa sasa acha nikapambane huko kwanza,” alisema Baba yake ingawa tumejiridhisha Yanga wiki iliyopita wamepambana kumshawishi mara kadhaa lakini bado amewawekea ngumu kwa kutotaja kiwango anachotaka wala kuwapa matumaini ya kuendelea kumsikilizia kabla dirisha halijafungwa.
“Mambo yakikamilika tutaweka wazi lakini wanamichezo wajue sasa hivi Msuva kucheza hapa nyumbani hapana acha akapambane kama ambavyo anahitaji yeye,” alisema huku Simba nao wakidai kuzungumza na mchezaji huyo wiki hii ingawa hawakufikia mwafaka wowote.Sio mara ya kwanza staa huyo mkali wa kufumaniwa nyavu kuhusishwa na wanajangwani hao, lakini wameongeza nguvu kutokana na uhitaji uliopo kwenye safu ya ushambuliaji hasa baada ya kuondoka Kwa Fiston Mayele.
Kwa mujibu wa TFF, Yanga inaweza kumuingiza Msuva kwenye usajili wao wa CAF kwa faini, lakini ni kama utetezi wao utakubalika.