Bacca afichua siri Yanga

Muktasari:

  • Mwanaspoti limezungumza na kocha mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alifichua ana mabeki bora ambao wanacheza kwa umoja na maelewano makubwa.

ACHANA na ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Yanga juzi nyumbani uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya 'Wasauzi' Marumo Gallants, habari ya mjini ni safu ya ulinzi ya timub hiyo, huku staa wa sasa wa nafasi hiyo, Ibrahim Bacca sambamba na kocha Nasreddine Nabi walifichua siri ya kucheza jumla ya dakika 540 bila kuruhusu bao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Ndio. Yanga imecheza mfululizo mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika ambazo ni sawa na dakika 540 bila kuruhusu bao hata moja huku ukuta wake unaoundwa na makipa Djigui Diarra na Metacha Mnata, mabeki Kibwana Shomari, Djuma Shabani, Joyce Lomalisa, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Abdallah 'Bacca' wakicheza kwa maelewano makubwa.
Mechi hizo ni dhidi ya Real Bamako (2-0), Monastir (2-0), TP Mazembe (1-0), Rivers United 2-0 na 0-0, na ile ya juzi Marumo akifa kwa Mkapa 2-0.

Mwanaspoti limezungumza na kocha mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alifichua ana mabeki bora ambao wanacheza kwa umoja na maelewano makubwa.

"Mabeki wetu wanacheza kwa umoja, wanaendeleza kile tunachowaelekeza mazoezini ni furaha kuwa nao kwa pamoja na naamini wanazidi kuimarika na kuelewana siku hadi siku," alisema Nabi anayesifika kwa mbinu na kuwasoma wapinzani.
Kwa upande Bacca ambaye licha ya ugeni wake kikosini, lakini ameingia moja kwa moja kwenye ukuta wa chama hilo na kuonyesha kiwango cha juu na hapa anaweka wazi siri kubwa ya ubora wao.

"Beki ni eneo linalohitaji umakini wa hali ya juu kwani ukikosea tu unaweza kuigharimu timu.
Nilivyokuja Yanga niliwakuta mabeki hawa wakicheza vizuri na kujipa muda wa kupata nafasi na sasa nashukuru ninacheza," alisema Bacca na kuongeza;

"Nadhani siri kubwa ni kujituma na kujitoa kwaajili ya timu, ukituangalia wote tunafanya hivyo na kila mmoja kwa nafasi yake anahakikisha hafanyi makosa na hata yakitokea basi anayasawazisha kwa haraka au mwingine anafanya hivyo. Nadhani umoja wetu ndio siri kubwa."

Baada ya mapumziko ya siku moja,  Yanga leo itarejea kambini kujiandaa na mechi ijayo ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji leo  Jumamosi uwanja wa Azam Complex na baada ya hapo kikosi kitasafiri hadi Afrika kusini kucheza mechi ya marudiano na Marumo Gallants.

Katika mechi hiyo na Marumo, Yanga inahitaji ushindi au sare ya aina yeyote ili kutinga kwa mara ya kwanza fainali ya michuano hiyo kwani ina faida ya mabao 2-0 iliyoyapata juzi kwa Mkapa.