Banda mguu ndani, nje Simba SC

Dar es Salaam. Simba inacheza mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca leo usiku, lakini Wekundu wa Msimbazi wanapiga hesabu za usajili kwa ajili ya msimu ujao, huku nyota wake, Peter Banda akiwa mguu ndani mguu nje.

Mechi ya kesho ni ya kukamilisha ratiba kwa Simba na Raja, kwani timu hizo zimefuzu robo fainali kutoka Kundi C na kuzibwaga Horoya ya Guinea na Vipers ya Uganda, ambazo nazo zitakutana kukamilisha ratiba.

Licha ya kwamba Simba inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo ili kuweka heshima, lakini mawazo makubwa ya benchi la ufundi ni juu ya hatua ya robo fainali, Ligi Kuu, na Kombe la TFF (ASFC) zinazofuata sambamba na usajili wa msimu ujao na tayari wameanza kufanya uchambuzi na machaguo ya wachezaji.

Katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu Afcon 2023 ugenini dhidi ya Misri, Banda aliingia kipindi cha pili na kutoka dakika ya 60 baada ya kuumia, wakati Malawi ikichapwa 2-0, hali iliyomtokea tena kwenye mechi ya marudiano wakifungwa 4-0, ambayo alianza katika kikosi cha kwanza na kutoka dakika ya sita baada ya kuumia tena na sasa madaktari wa Simba wanamsubiri ili watoe ripoti ya afya yake.

Tayari kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameanza kuandaa ripoti ya kikosi chake, ambayo inatarajia kuwa na mabadiliko makubwa kwa wachezaji na pia kutazama nyota wengine nje ya timu, ambao anaweza kuwasajili katika dirisha lijalo la msimu ujao.

Chanzo cha kuaminika ndani ya Simba kilidai kuwa Robertinho ameuambia uongozi hata kabla msimu haujaisha, anahitaji winga mmoja wa kimataifa na tayari amewapa majina yasiyopungua matatu ili waanze kuwafuatilia, wakati majina ya Banda na beki Mohamed Ouattara yakiwa hatarini.

“Kocha anataka wachezaji wapya akiwemo winga mmoja hatari wa kigeni, lakini pia kuna wachezaji nafasi zao kuondoka zimekuwa kubwa kutokana na myenendo yao na Banda ni mmojawapo, kwani muda mwingi amekuwa majeruhi na kushindwa kuisaidia timu.

“Kwa kuwa bado mechi zinaendelea, siwezi kuthibitisha nani na nani wataondoka, lakini kuna mabadiliko makubwa tutayafanya mwishoni mwa msimu huu,” kilieleza chanzo hicho.

Hadi sasa, Simba ina wachezaji 12 wa kigeni, idadi kamili ya wanaoruhusiwa kusajiliwa na klabu za Ligi Kuu, ambao ni Henock Inonga, Joashi Onyango, Mohamed Ouattara, Ismael Sawadogo, Sadio Kanoute, Clatous Chama, Jean Baleke, Moses Phiri, Pape Sakho, Saidi Ntibanzokiza, Augustine Okrah na Banda.