Biashara yaipunguza kasi Yanga, Mayele atetema tena

Monday May 23 2022
full pic
By Damian Masyenene

LICHA ya kushindwa kuondoka na pointi tatu dhidi ya Biashara United leo bado Yanga imezidi kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC ikibakiza pointi tatu tu itangazwe bingwa.

Yanga ambayo ilikuwa inahitaji pointi tano tu katika michezo mitano iliyosalia leo imekwaa kisiki bada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Hivyo hesabu zinabaki pointi tatu tu katika mechi nne zijazo ili kujihakikishia ubingwa huo.

Yanga imeambulia sare hiyo baada ya washindani wake wakubwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu, Simba nayo kulazimishwa sare ya 1-1 na Geita Gold uwanjani hapi jana.

Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao mnamo dakika ya 74 likifungwa na Fiston Mayele kwa jitihada binafsi akiunganisha mpira mrefu uliopigwa na Djuma Shaban.

Dakika tatu baadae Biashara United ikasawazisha bao hilo katika dakika ya 77 likifungwa na Opare Collins aliyetumia vyema makosa ya walinzi wa Yanga kushindwa kuuokoa mpira wa hatari uliokuwa unazengea kwenye lango lao.

Advertisement

Baada ya sare hiyo Yanga inaendelea kukaa kileleni ikifikisha pointi 61 huku Biashara United ikifikisha alama 24.

Nyota wa Yanga Fiston Mayele amefikisha bao la 14 na kumfikia mshindani wake George Mpole aliye na mabao 14.

Advertisement