Bilionea wa A. Kusini autaka urais CAF

Muktasari:

Uamuzi wa Motsepe kuwania urais ulitangazwa na Chama cha Soka cha Afrika Kusini (Safa) na anakuwa mtu wa pili kupambana na rais wa sasa, Ahma Ahmad baada ya Jacque Anouma wa Ivory Coast.

Johannesburg, Afrika Kusini. Bilionea wa Afrika Kusini, Patrice Motsepe atagombea urais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Machi, chama cha soka cha nchi hiyo, Safa kimetangaza leo Jumatatu (Novemba 9).
Bilionea huyo anamiliki klabu ya jijini Pretoria ya Mamelodi Sundowns, ambayo imekuwa moja ya klabu kumi bora barani Afrika kwa miaka kadhaa na mwaka jana ilitwaa mataji matatu ya Afrika Kusini, ukiwemo ubingwa nchi.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes utajiri wa Motsepe una thamani ya dola 2.2 bilioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh4.5 trilioni za Kitanzania)
Motsepe alitengeneza utajiri wake katika sekta ya madini.Bilionea huyo pekee mweusi nchini Afrika Kusini ana hisa katika klabu ya raga.
Motsepe pia alinunua asilimia 37 ya hisa za kampuni ya Blue Bulls kwa kiwango cha fedha ambacho hakijawekwa bayana.
Timu yake ya mchezo wa raga inatumia uwanja mmoja na klabu ya Mamelodi Sundowns.
Uamuzi wake umefanya idadi ya watu waliojitokeza kugombea nafasi hiyo ya juu katika soka barani Afrika, kufikia watatu, baada ya rais wa sasa, Ahmad Ahmad kutoka Madagascar na Jacques Anouma kutoka Ivory Coast kutangaza uamuzi wao.
Ahmad alisema mwezi uliopita kuwa atagombea kwa mara ya pili urais wa CAF ambao ni wa miaka minne kwa kila kipindi, baada ya kufanikiwa kumuondoa Issa Hayatou kutoka Cameroon ambaye aliliongoza shirikisho hilo kwa miaka 29. Katika uchaguzi, Ahmad alipata kura 34 dhidi ya 20 za mkongwe huyo katika uongozi wa soka Afrika, miaka mitatu iliyopita.
Anouma, ambaye alizuiwa kugombea urais wa CAF mwaka 2013 wakati mpango ulioratibiwa na Hayatou ulipofanikisha kufanya mabadiliko ya sheria yaliyomzuia raia huyo wa Ivory Coast kugombea, alitangaza uamuzi wa kugombea nafasi hiyo mwishoni mwa wiki.
Motsepe hakuhudhuria mkutano na waandishi wa habari jijini Johannesburg ambako taarifa yake ya kugombea ilitolewa kwa kuwa yuko katika karantini baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Rais wa Safa, Danny Jordaan alitangaza uamuzi huo akiwa pamoja na waziri wa michezo, Nathi Mthethwa.
"Ni mtu sahihi kuliko wote ambao tungeweza kuwatoa kwa ajili ya uongozi wa CAF. Hatutaki muafaka katika uongozi au maadili," alisema Jordaan ambaye ni makamu wa tatu wa rais wa CAF.
Marais wa vyama vya soka vya Nigeria na Sierra Leone, Amaju Pinnick na Isha Johansen, walikuwa jijini Johannesburg wakati uamuzi huo ukitangazwa.
Pinnick, ambaye alidokeza mwezi uliopita kuwa angeweza kugombea nafasi hiyo, alithibitisha kuwa hatagombea na badala yake atamuunga mkono Motsepe.
Pinnick, ambaye alikuwa makamu wa rais wa CAF, alitimuliwa na Ahmad baada ya kutofautiana kuhusu mwelekeo wa shirikisho hilo lenye makao yake makuu jijini Cairo.
Nchi 46 ziliripotiwa mwezi uliopita kuwa zimemuandikia barua Ahmad kumueleza kuwa zitamuunga mkono katika harakati zake za kutetea nafasi ya urais wa CAF.
Lakini nchi nane hazikutajwa katika orodha hiyo ambazo ni Algeria, Botswana, Ivory Coast, Nigeria, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe.