Carragher, Owen wataja mechi ya kuipa Arsenal ubingwa EPL
Muktasari:
- Arsenal inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu ikiwa na pointi 76 ilizokusanya katika michezo 35.
Baada ya Man City kulazimishwa sare ya mabao 3-3 nyumbani na Everton jana Jumatatu, Mei 2, 2026, nyota wawili wa zamani wa Liverpool na England, Michael Owen na Jamie Carragher wanaamini kwamba matokeo hayo yanaiweka Arsenal katika nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.
Na wawili hao wameitaja mechi dhidi ya West Ham Jumapili ijayo kama ndio utaihakikishia ubingwa Arsenal ikiwa itapata ushindi.
Wakizungumza mara baada ya Man City kuangusha pointi mbili katika mchezo dhidi ya Everton jana, Owen na Carragher wamesema kuwa kwa sasa Arsenal haitokuwa na cha kujitetea ikiwa haitotwaa taji la EPL kwa vile sasa inahitajika kushinda mechi zake tu.
“Kama Arsenal itapata ushindi dhidi ya West Ham Jumapili ijayo, wanashinda ligi. Unaweza kufikiria uwanja utakavyokuwa kesho (leo) dhidi ya Atletico Madrid katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Kuingia katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi kuwa mikononi mwako huku ukiwa umebakiza mechi tatu mkononi,” amesema Carragher.
Owen kwa upande wake amesema kuwa Arsenal hawapaswi tena kufanya makosa katika mechi zilizobakia hasa dhidi ya West Ham United.
“West Ham watakuwa na cha kuonyesha katika mechi hiyo. Hakuna kitakachoizuia Arsenal kama itaifunga West Ham,” amesema Owen.
Kwa upande wake mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry amesema kwamba japo timu yake ina nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, hawezi kufurahia hadi pale itakapojihakikishia taji hilo.
“Sasa imebaki mikononi mwa Arsenal. Haipo tena mikononi mwa Man City. Nilisema mwanzo kuwa naona (Man) City ikiangusha pointi dhidi ya Everton na ndio maana nina wasiwasi na mechi dhidi ya West Ham.
“Hivyo kwa sasa nakaa katika mstari wangu na sishangilii mapema kwa sababu bado haijatimia, lakini naona ikitokea,” amesema Henry.