Chama abeba matumaini Singida BS
Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesifu usajili wa kiungo Clatous Chama uliofanywa na timu yake katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea ambalo litafikia tamati Septemba 7, mwaka huu.
Chama amejiunga na Singida Black Stars akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Yanga aliyoitumikia kwa msimu mmoja tu.
Ingawa bado klabu hiyo haijamtambulisha rasmi nyota huyo kutoka Zambia, Gamondi amesema kuwa uwepo wa Chama utaongeza kitu kikubwa katika kikosi chake hasa ubunifu jirani na lango la timu pinzani.
Gamondi amesema kuwa mchezo wa Kombe la Kagame ambao wamecheza dhidi ya Coffee ya Ethiopia umeonyesha uhitaji wa Chama katika kikosi chake.
"Sijafurahishwa na kiwango tulichoonyesha hasa katika eneo la kushambulia ambalo tulikosa mpango wa kuwafungua wapinzani wetu. Ni jambo tunalotakiwa kuimarika na uwepo wa mchezaji kama Clatous Chama utakuwa na msaada mkubwa katika kuongeza ubunifu kwenye eneo la ushambuliaji.
"Kujiunga kwake (Chama) akiungana na wachezaji wengine ambao wapo na majukumu ya timu za taifa kama Aucho (Khalid) na Tchakei (Marouf) naamini utaongeza kitu kikubwa kikosini na tutaimarika zaidi," alisema Gamondi.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza amethibitisha kuwa Chama amenaswa na timu hiyo na ataungana na timu hiyo jana au leo.
"Uzoefu na ubora ndio vitu viwili ambavyo vinakwenda kuongezeka kwenye timu. Chama nadhani anaweza kuwasili kesho (jana) mapema. Anaungana nasi hapa naye atapata muda wa kuungana na timu naye atafanya mazoezi.
"Tupo katika sehemu ya maandalizi ya msimu. Hii ni sehemu ya pili ya maandalizi ya msimu mpya. Wachezaji wengi ambao tupo nao katika kikosi ni wageni na Kocha Miguel Gamondi na benchi lake la ufundi, wanaendelea kutengeneza mifumo mizuri. Muda ukifika, moto wa Singida Black Stars mtauona vizuri," alisema Masanza.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Chama alihusika na mabao tisa ya Yanga ambapo alifunga mabao sita na kupiga pasi tatu za mwisho.
Katika kikosi cha Singida Black Stars, Chama anachukua nafasi ya Arthur Bada ambaye ameuzwa na timu hiyo kwenda JS Kabylie ya Algeria.