Chama apiga mkwara

KIUNGO fundi wa Simba, Clatous Chama amesema msimu ujao timu yao itakuwa katika kiwango bora kulingana na maandalizi ambayo wamekuwa wakiyapata Misri, lakini akasema kwa Mkapa pia patachimbika.

Simba na Yanga zitakutana Agosti 13, Dar es Salaam kukata utepe mchezo wa Ngao ya Jamii.

Chama amesema hakumaliza msimu uliopita vizuri kutokana na kupata majeraha, ila baada ya matibabu mazuri ameimarika na kupona kabisa.

Amesema mashabiki wa Simba hawakuonekana kuwa na furaha kutokana timu yao kutofanya vizuri msimu uliopita, huku wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mataji mengi misimu minne nyuma na sasa mambo yanarudi upya.

“Huu msimu ambao unaanza ni kama kauli ya bondia Karim Mandonga vile tunakwenda kufanya kazi, basi hilo ndilo tumekubaliana wachezaji Simba. Tunahitaji kufanya vizuri,” alisema.

“Nafahamu watu wanaamini naweza kufanya kitu kutokana na uwezo wangu, tuombe muda ufike kila kitu kitakuwa sawa kwenye mechi nyingi kufanya kama vile ambavyo wao wanahitaji kutoka kwangu.

“Kutokana na ukubwa wa Simba halitakuwa jambo zuri kuona tunashindwa kufanya vizuri misimu miwili mfululizo. Kiukweli kikosi cha wakati huu kimeimarika mchezaji mmoja mmoja na timu nzima. Ukitaka kuamini vizuri haya maneno yangu nawaomba mashabiki wa Simba wajitokeze siku ya Wiki ya Simba.”