Chama atawala mapokezi ya Yanga

Muktasari:

  • JINA la Clatous Chama ndilo lililotawala jana wakati wa mapokezi ya timu ya Yanga ilipowasili kwa ndege kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe, mashabiki wakisema wanamtaka staa huyo wa zamani wa Simba atue Jangwani na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa, amewatuliza na bonge la tabasamu.

MBEYA. JINA la Clatous Chama ndilo lililotawala jana wakati wa mapokezi ya timu ya Yanga ilipowasili kwa ndege kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe, mashabiki wakisema wanamtaka staa huyo wa zamani wa Simba atue Jangwani na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa, amewatuliza na bonge la tabasamu.

Yanga waliwasili jana kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya Kwanza unaotarajiwa kupigwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Sokoine jijiji hapa na kupokewa na mashabiki wengi.

Ilikuwa hivi, baada ya timu kutua, Senzo ndiye alitokea mapema akiwa wa kwanza na akapokewa na bonge la shangwe kutoka kwa mashabiki waliokuwa wamefurika viwanjani hapo kwa mapokezi.

Baada ya kufika Senzo aliwapungia mkono akionyesha sura ya furaha, ambapo mashabiki walilipuka na kumtaja Chama wakisema wanamtaka Jangwani.

Kelele zilitawala uwanjani hapo na kuwafanya makomandoo kuwatuliza wakiwapanga maeneo rafiki, huku wakitoa masharti kuwa hakuna kumgusa mchezaji kwa namna yoyote.

“Tunamtaka Chama, tunamtaka Chama, tunamtaka Chama....” zilisikika shangwe na kelele kutoka kwa mashabiki wakimlenga Senzo.

Hata hivyo, Mtendaji huyo aliyekuwa amevalia suti michezo ya rangi yenye rangi za njano na kijani za Yanga, aliwatuliza kwa kuwaoa bonge la tabasamu bila kuongea chochote hadi wanaondoka maeneo hayo kwenda hotelini walipofikia, Tughimbe.

Habari kubwa inayotawala soka la Bongo katika siku za karibuni ni uvumi kuhusu hali ya baadaye ya Chama akidaiwa kuwa mbioni kurejea nchini huku Simba na Yanga zikitajwa kuwa huenda akajiunga na mojawapo.

Simba ilimuuza Chama katika timu ya RS Berkane inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, ambapo inaelezwa kuwa Yanga wanahaha sana kuhakikisha wanainasa saini ya staa huyo, lakini vigogo wa Simba wakitamba kwamba kama Mzambia huyo atarudi Tanzania basi atatua Msimbazi tu na si kwingineko.

Yanga iliwasili kwa ndege ya Air Tanzania saa 2 asubuhi ambapo walitarajia kufanya mazoezi jioni katika uwanja wa Jeshi uliopo mtaa wa Itende jijini hapa kisha kuendelea na programu.

Yanga haijapoteza mchezo msimu huu