Che Malone atoa kauli nzito Simba
Dar es Salaam. Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba akitokea Coton Sports ya Cameroon, beki Che Malone Fondoh amefunguka akisema amekuja kwa ajili ya kuwapa furaha Wanasimba.
Malone aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Cameroon kwa msimu uliopita ni miongoni mwa nyota wapya walioikamua Simba, kwani ililazimika kuvunja mkataba ili kumpata.
Simba imetambulisha wachezaji wengine wapya wa kigeni, mshambuliaji Willy Onana (Cameroon) aliyeibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda akiichezea Rayon Sports na winga wa Ivory Coast, Aubin Kramo kutoka Asec Mimosac.
Akizungumza na Mwananchi jana, Malone ameeleza furaha yake kujiunga na Simba, huku akiweka wazi kuwa na deni la kuwapa mafanikio wanachama na mashabiki wa Msimbazi.
"Nafurahi kujiunga na Simba, ni timu kubwa inayofanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika. Napaswa kujituma na kufanya vizuri zaidi ili nisiwaangushe bali kuwaheshimishe," alisema Malone.
Katika hatua nyingine, beki huyo mwenye miaka 24, anayetarajiwa kutengeneza pacha ya ukuta imara wa Simba na Henock Inonga, alisema anaamini umoja, kujituma na ubora wa kikosi kizima ndiyo utaifanya Simba kuwa tishio zaidi kwa msimu ujao.
Katika hatua nyingine, Simba imewaongeza mkataba wa miaka miwili mabeki wake, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, ambao watabaki Msimbazi hadi 2025.
Wakati Simba ikifanya hivyo, kikosi chake kinaondoka saa 5 asubuhi ya leo kwenda Uturuki kwa ajili ya kuanza kambi ya takribani wiki tatu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.