Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cunha, Vinicius wang'ara, Brazil ikiishushia Haiti dhoruba

Muktasari:

  • Brazil ilikuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza wa Kombe la Dunia la mwaka 2026, baada ya mechi ya kwanza ya ufunguzi kuonyesha kiwango kibovu na kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Morocco.

PHILADELPHIA, MAREKANI: MABINGWA mara tano na vinara wa Kombe la Dunia, timu ya taifa ya Brazil 'Selecao', imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0, dhidi ya Haiti katika mechi ya pili ya kundi C, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Philadelphia, Pennsylvania, Marekani.

Brazil ilikuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza wa Kombe la Dunia la mwaka 2026, baada ya mechi ya kwanza ya ufunguzi kuonyesha kiwango kibovu na kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Morocco.

Katika mechi hiyo ya leo, Brazil ilitumia vyema dakika 45, za kipindi cha kwanza baada ya kufunga mabao yote matatu, yaliyofungwa na Matheus Cunha aliyefunga mawili dakika ya 23, kisha kuongeza la pili dakika ya 36, akimalizia pasi nzuri ya Vinicius Junior.

Dakika ya 45+3, kabla ya mapumziko, Vinicius Junior akaifungia Brazil bao la tatu na la kwanza kwake katika mechi ya leo, akitumia vyema pasi ya nyota wa kikosi hicho, Lucas Paqueta na kuipeleka mapumziko timu hiyo ikiwa kifua mbele na uongozi wa mabao 3-0.

Kipindi cha pili Haiti iliingia na mkakati mzuri wa kuzuia huku ikitengeneza mashambulizi ya kushtukiza na hadi dakika 90, zinakamilika Brazil ikanufaika na mabao matatu ya kipindi cha kwanza.

Kichapo hicho cha Haiti kinakuwa ni cha pili mfululizo katika kundi lake la C baada ya mechi ya kwanza ya ufunguzi pia kupoteza bao 1-0, dhidi ya kikosi cha Scotland.

Ushindi huo unaifanya Brazil kuongoza kundi C na pointi nne ambazo ni sawa na Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku Scotland ikiwa ya tatu na pointi tatu, wakati Haiti inaburuza mkiani ikiwa haina pointi zozote hadi sasa.

Historia ya Brazil katika Michuano ya Kombe la Dunia ni ya kipekee kwa sababu ndio timu yenye mafanikio makubwa zaidi kwenye mashindano hayo, huku ikiwa pia ni taifa lililoshiriki Kombe la Dunia tangu lilipoanza rasmi Uruguay mwaka 1930.

Brazil ndilo taifa linaloongoza kuchukua Kombe la Dunia mara nyingi ikichukua mara tano kuanzia mwaka 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002 kati ya fainali saba ilizofika, ikiwa ni rekodi ya kuvutia inayoendelea kuishi katika kizazi cha timu hiyo.

Timu hiyo ilitwaa ubingwa wa kwanza wa Kombe la Dunia la mwaka 1958, baada ya kuifunga Sweden mabao 5-2, ambao walikuwa ndio wenyeji, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Rasunda ulipo mji wa Solna, karibu na mji mkuu wa Stockholm.

Katika Fainali hiyo iliyopigwa Juni 29, 1958, licha ya Brazil kuchukua taji la kwanza la Kombe la Dunia, ila ndio mechi iliyomtambulisha rasmi aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Edson Arantes do Nascimento 'Pele' aliyecheza akiwa na miaka 17.

Pele aliwika akiwa na umri mdogo wa miaka 17, baada ya kuifungia Brazil mabao mawili ya dakika ya 55 na 90, sawa pia na Edvaldo Izidio Neto maarufu 'Vava' aliyefunga dakika ya 9 na 32, huku lingine likifungwa na Mario Zagallo dakika ya 68.

Sweden iliyokuwa mwenyeji ilianza vizuri na kuishtukiza Brazil kwa kuifunga bao la mapema dakika ya nne, lililofungwa na Nils Liedholm na lingine moja likifungwa na Agne Simonsson dakika ya 80, japo mwisho wa mechi hiyo ilichapwa mabao 5-2.

Katika mataji matano iliyochukua Brazil, mawili iliyachukua kwenye nchi zinazoandaa kwa sasa Kombe la Dunia, ambazo ni Marekani na Mexico ukiiondoa Canada ambao ni waandaaji pia, jambo linalosubiriwa kuona kama rekodi hiyo itajirudia tena.

Kombe la Dunia la mwaka 1970, lililofanyika Mexico, Brazil ilishinda taji hilo likiwa ni la tatu kwake baada ya kuchukua mwaka 1958 na 1962, ambapo katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azteca Juni 21, 1970, iliichapa Italia mabao 4-1.

Fainali za Kombe la Dunia la Marekani mwaka 1994, Brazil ikatwaa tena taji hilo likiwa ni la nne kwake katika historia, ikiifunga Italia kwa penalti 3-2, baada ya mechi hiyo iliyopigwa Julai 17, 1994, kuisha kwa suluhu ya (0-0), dakika 120.

Mara ya mwisho kwa Brazil kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 2002, katika fainali zilizofanyika nchi mbili za Japan na Korea Kusini, ambapo timu hiyo iliifunga Ujerumani mabao 2-0, Juni 30, 2002 na kuchukua taji hilo la tano.

Licha ya mafanikio hayo, ila moja ya rekodi mbovu inayokumbukwa na wadau wa soka kwa Brazil ni ya kuchapwa mabao 7-1, dhidi ya Ujerumani ikiwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2014, katika hatua ya nusu fainali iliyopigwa Julai 8, 2014.

Kwa upande wa Haiti ni moja ya mataifa ya Karibiani yanayojulikana sana kwa mapenzi ya soka, lakini historia yao katika Kombe la Dunia sio ya kuvutia, huku ikishiriki mara ya kwanza michuano ya mwaka 1974, iliyofanyika Ujerumani Magharibi.

Katika ushiriki wake wa kwanza, Haiti ikaangukia kundi la nne la kifo lililokuwa na timu za Italia, Argentina na Poland, ambapo kikosi hicho kilipoteza mechi zote tatu, huku kikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14.

Mabao yote mawili ya Haiti yalifungwa na mshambuliaji, Emmanuel Sanon huku bao lililompa heshima na kukumbukwa zaidi ni aliloifunga Italia, kwani lilivunja rekodi ya kipa wa timu hiyo, Dino Zoff ya kucheza dakika 1142 bila ya kuruhusu bao.

Tangu iliposhiriki mwaka 1974, timu hiyo imerejea tena Kombe la Dunia la 2026, baada ya kupita miaka 52, ikiwa ni mara ya pili kwa kikosi hicho kushiriki, huku kikiwa hakipewi nafasi zaidi ya kufanya vizuri kutokana na ushindani uliopo.