Diamond kisiki, lakini hapa dhaifu

"Alikuja kwangu 2008, akaniambia Mkubwa Fella, naomba uwe meneja wangu, nilimkatalia nikamwambia na wewe unataka kunitukana kama wenzako," ndivyo anaanza kusimulia Mkubwa Fella, akiweka bayana namna alivyokutana na Diamond.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Fella anaeleza namna ambavyo haikuwa rahisi kukubali ombi la kuwa meneja wa Diamond.

“Nilikuwa nimetoka kuvurugana na wasanii, tena baadhi walinitukana sana, sikutaka kumsimamia tena msanii, hivyo nilimwambia Diamond anipe miezi mitatu ya kujifikiria. "Baada ya miezi mitatu, alirudi tena, hapo ndipo niliona yuko 'serious' ila nilimuuliza na wewe unataka kunitukana kama walivyofanya waliotangulia? Akaniambia Mkubwa, watu hawafahamu tu, lakini mimi naona nyota na uwezo uliokuwa kwenye muziki, japo kuna watu wanakuchukulia juujuu," anasema.
 

Miaka 15 na Diamond

"Ninachofarijika, Diamond hajawahi kuharibu wala kuniangusha, ukimuona Naseeb (Diamond) kwenye picha unakuwa na mawazo naye tofauti, lakini ukibahatika kukaa naye, utaona kuna tofauti kubwa sana.

"Kwanza ni msaidizi wa watu na msikivu, ukimuonya anajua nini unamaanisha, sio aina ya wasanii ambaye hata ukimwambia wee! hasikii na kukuona miyeyusho.
"Diamond pamoja na umaarufu wote, lakini anaonyeka, anaheshimu na kuona huyu ni meneja wangu, hivyo anasikiliza, shida yake ni moja tu, wanawake.

"Nilishamwambia sana, wewe angalia zaidi kazi yako, hawa wanawake wapo tu na wanazaliwa kila siku, hivyo heshimu kazi, nakumbuka kuna siku alitaka kuharibu kazi sababu ya mwanamke.
"Babu Tale alizungumza naye lakini hawakuelewana, nikaambiwa mimi, wakati huo niko nyumbani kwangu Kilungule, siku hiyo alitakiwa asafairi kwenda Afrika Kusini kwenye shoo.

"Alikuwa bado anaishi Kijitonyama, nikamfuata nikamwamsha nikamwambia muda huu unatakiwa kuripoti uwanja wa ndege, vaa nguo, panda bodaboda ukawahi ndege, alikuwa na mwanamke wake, akataka kuacha kazi ya watu, hilo ndilo tatizo lake kubwa," anasema Fella ambaye ni meneja wa kwanza wa msanii huyo, kisha Tale na Salaam ambao wote yupo nao.

Anasema yeye kwa Diamond sio kama mchungaji wa ng'ombe, kwamba atakuwa nyuma muda wote, hapana, kwani umeneja wa hivyo ulikuwa zamani.
"Katika maisha yangu ya kuwa kwenye muziki, sijawahi kuishi maisha mazuri kama ya sasa nikiwa namsimamia Diamond, ananilipa mshahara kila mwezi, nilipotoka ni kama bakuli, sasa niko na sufuria."
 

Nature amuingiza kwenye muziki

Fella anasema, hajawahi kuamini kwenye kushindwa na kila siku ndoto yake ni kufanya kitu kipya, kwani hata baada ya kushindwana na Nature hakurudi nyuma.
"Mimi nilikuwa naishi Sauzi (Afrika Kusini), Nature aliponishirikisha masuala yake nikasema ngoja nimsaidie, mwanzo ilikuwa si biashara, lakini baadaye ikaja kuwa hivyo.
"Nikiwa hapa nchini, kwangu ilikuwa Kurasini, Nature kama mdogo wangu wa mtaani nilikuwa namsaidia mambo yake ya shule, lakini wakati huo pia alikuwa mpenzi sana wa mpira, ni mchezaji mzuri, hivyo nilimsaidia kwenye mambo ya shule na mpira.
"Baadaye akaniambia anataka kuimba, tukaenda naye kwa P Funky (Majani) kule tukatengeneza mikataba nikawa namsimamia, hapo ndipo nilianza kuingia kwenye muziki hadi sasa," anasema.


Mambo sita aliyoanzisha kwenye muziki nchini

"Nilianza na Nature, mimi ndiye msimamizi wake wa kwanza na meneja wa kwanza, wakati huo wanamuziki hawakuwa na mameneja.
"Nilianzisha kundi la kwanza la Muziki la TMK Family, kabla hakukuwa na makundi ya muziki, japo tulipishana kauli baadaye likatengenezwa Wanaume Halisi, hata hivyo bado TKM ikaendelea kuwa bora.
Anasema ili kuonyesha hakubahatisha, akatengeneza msanii mdogo (Dogo Asley) aliyeanza kuimba wimbo wake wa ‘Naenda kusema kwa mama’.

"Kipande anachoonekana mzee Pembe katika huo wimbo, ile ni sauti yangu, niliingiza Pembe akaigiza kile kipande, lakini kingine nilichokianzisha ni kundi la Yamoto Band ambalo liliwatoa wanamuziki wadogo, kisha kuanzisha kundi la madada sita.

"Kingine ni kumuibua na kumtengeneza bibi Cheka hadi kuwa bora na kupata umaarufu uzeeni, ametangulia mbele za haki, Mwenyezi Mungu amrehemu, alinitafuta wakati huo pale maskani yetu TMK.

"Kabla ya kuonana naye, alinipigia simu na kunieleza yuko Bunju, nikamwambia tafuta nafasi uje TMK, kweli nilifanya naye kazi, lakini baadaye akapata wajuaji, wenye mipango zaidi, hawakujua kama bibi namtengeneza vipi na studio tulifanya nini hadi bibi anaimba, wakaingilia lakini ndiyo dunia ilivyo."
 

Yamoto yarudi upya

Baada ya anguko la Yamoto Band, Fella anasema sasa kuna Yamoto Music ambayo ni mbadala wa kundi hilo ambalo anasema hataki kuzungumzia sana anguko lake.

"Ukiangalia, Yamoto Band ilianza 2004 na kufa 2006, ni miaka miwili tu, lakini ilikuwa na kitu kikubwa hadi watu kujiuliza kwa nini kila ninachokifanya kinang'aa, wakaona nao waingize mkono huko wakitarajia kunirudisha nyuma, wanasahau ukinirudisha miezi miwili ule wa tatu tunakutana tena mjini.

"Nilisakwamwa vitu vingi kuhusu hili kundi, nikaambiwa hata nyumba sikuwajengea, lakini kuna mmoja ni juzijuzi tu amekwenda kuiuza nyumba ile, mwingine amemweka mjomba wake anaishi na mwingine kamweka mama yake, lakini sikutaka malumbano, nikakaa kando.

"Hivi sasa kuna Yamoto Music, wametoa nyimbo mpya inaitwa ‘Snitch sio mwana,’ ni kundi ambalo linakuja kwa kasi na bahati nzuri nafahamu njia zote za kupita ili ku'shine (kung’aa), nakumbuka Shaa alifanyiwa video kubwa kubwa lakini haku-shine.

"Nikamwambia Master Jay nipe miezi mitatu huyu namweka juu, kweli akatoa wimbo wa ‘Sugua gaga’, alishangaa akanifuata anasema aisee Mkubwa nini kimetokea? Nikamwambia ahaa, baki na mkeo," anasema Fella kwa utani akitaka kuonyesha namna ambavyo ana uwezo wa kumng’arisha msanii yeyote nchini.
Anasema huwa anaumizwa na watu wengi kutozungumza ukweli, akitolea mfano changamoto alizopitia kuwasimamia baadhi ya wasanii huku lawama nyingi akitupiwa yeye.
"Utakuta msanii anakuja kwako, msingi alionao ni wazo tu, meneja anamtengeneza, tengeneza audio, video na kisha anafanikiwa halafu mwisho wa siku anasema anadhulumiwa.
"Hii hali imeniumiza mno, kuna muda nawaza hivi Mwenyezi Mungu ndiyo kanipangia hivi? Sijawahi kuingia kwenye muziki kutafuta faida, lakini sasa moja kwa moja inakuja tu kwa Diamond, nakumbuka nyuma wakati wa TMK tulikuwa tunapata laki nane wakati huo mko 14 na huenda mko nje ya Dar es Salaam, hiyo pesa mnaigawanaje? halafu mtu anakwambia unamdhulumu! Inaumiza sana.”
 

Ingizo jipya WCB

Fella anasema WCB itakuwa na ingizo jipya kutoka Temeke, ambaye anamtaja kuwa ni msanii mwenye kipaji, lakini atatambulishwa baada ya Zuchu, Mboso, Lavalava na Diamond mwenyewe kuachia ngoma zao mpya.
"Ni msanii wa singeli, huyu mtoto ana kipaji wapenzi wa WCB wakae mkao wa kula," alisema Fella akifafanua pia tetesi za Queen Dareen kuondoka WCB.
"Hajaondoka, bado yupo, ingawa ni kwa nini hajaachia wimbo mpya kwa muda mrefu, hilo ni suala lake binafsi, lakini yupo," anasema.
 

WCB kurudi kwenye tuzo za TMA

Baada ya kususia mwaka jana, mwaka huu, Zuchu na Mboso wameingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania Tuzo za Muziki Tanzania, ambazo Fella anasema wameingia ili kuona hatima ya tuzo hizo.
"Nyuma zilikuwa kama zinatolewa kwa wivu, ila mwaka huu WCB tumeona tumsapoti mama na kuingia, wacha tuangalie hatma yake, japo wameingiza nyimbo nyingine ambazo zimefanya vizuri hawajaziweka, ila wacha twende nazo mdogo mdogo tunaamini huko mbeleni mambo yatakwenda vizuri zaidi.
 

Hakuwa na ndoto za udiwani

Mkubwa Fella ni Diwani wa kata ya Kilungule kwa muhula wa pili sasa, ingawa awali alipojitosa kwenye siasa, baadhi ya watu walimnyooshea vidole na kuhisi hataweza.

"Unajua Mungu ni mkubwa sana, kwenye udiwani sikuw hata na 'interest' lakini mwisho wa siku akanipa kipawa hicho na wananchi wangu wa Kilungule wakanibeba, huu ni muhula wa pili, na kwenye uchaguzi uliopita wananchi ndiyo walinichukulia fomu.
"Waliona niliyoyafanya kwenye muhula wa kwanza, wakati wangu ndipo kwa Mpalange, barabara imejengwa, tumejenga hospitali, shule ya sekondari, msingi hadi watu wakashangaa na kuulizana hivi huyu ni yule M-bongo fleva au Fella gani?

"Mwanzoni walipata tabu kunielewa, walisema hivi huyu naye ataweza! Niko kwenye udiwani mwaka wa saba sasa, lakini karibu vitu vyote vya maendeleo kwenye kata yangu nimevimaliza, kuna barabara za zege na lami, hospitali, visima, madarasa, shule, kituo cha polisi ambacho nimejenga kwa pesa yangu ya mfukoni," anasema.