Djuma sasa rasmi Yanga miaka miwili

Thursday June 10 2021
YANGAPIC
By Khatimu Naheka

Yanga imefanikiwa kuipiga bao Simba baada ya kufanikiwa kumalizana na beki Mkongomani Djuma Shaban akitokea klabu ya AS Vita.

Usajili wa Djuma ambaye pia ni nahodha wa Vita umekamilishwa jana jioni jijini Kinshasa Yanga wakiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Mhandisi Hersi Said.

Hii inakuwa ni safari ya tatu kwa Hersi nchini Congo kukamilisha usajili wa mastaa wapya wa Yanga ambapo mapema kabla ya msimu huu kuanza alitua jijini hapo kuwasainisha winga Tuisila Kisinda kutoka klabu ya Union Maniema na nahodha msaidizi na  kiungo Mukoko Tonombe ambao waliongeza Makali ya Yanga baada ya kusajiliwa.

Djuma anakuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kusajiliwa kuelekea msimu ujao akisaini mkataba wa miaka miwili na Yanga .

Mbali na kumalizana na Djuma pia Hersi amemalizana pia na klabu yake ya Maniema ambao walimtoa kwa mkopo AS Vita.

Hatua hiyo ya Yanga ni kama imeipiga bao Simba waliokuwa wanamuwinda Djuma kwa muda mrefu kabla ya Yanga kuingilia kati na kumalizana naye.

Advertisement

Usajili huo wa Yanga sasa unamaanisha kwamba Djuma anakuja kuleta changamoto mpya kwa beki wa kulia wa timu hiyo Kibwana Shomari ambaye amecheza karibu michezo yote ya Yanga ya ligi msimu huu.

Endapo Djuma atafanikiwa kufanya vyema ndani ya Yanga timu hiyo itanufaika na ubora wa Djuma katika kupandisha mashambulizi na hata kufunga mabao.

Advertisement