EXCLUSIVE: Hersi atoboa siri, Msola kuitanguliza Yanga iko hivi...

EXCLUSIVE: Hersi atoboa siri, Msola kuitanguliza Yanga iko hivi...

JULA I 9, 2022, Hersi Said alitangazwa kupitishwa kwa kura zote na wanachama wa klabu ya Yanga African (Yanga Afrika) katika mkutano wa uchaguzi wao uliofanyika kwenye Ukumbi wa kimataifa wa Mwl Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mwananchi limefanya naye mahojiano maalumu na kuzungumzia mambo mbalimbali ndani ya klabu hiyo; “Nimekuwa Yanga katika maeneo tofauti kabla ya kuwa Rais hasa nikiwa sehemu ya udhamini na ufadhili, udhamini ambao ulikuwa na changamoto kubwa sana kwa sababu tuliikuta Yanga ikiwa katika mazingira magumu na kwa kuanzia hapo tukatakiwa tuiinue.

“Kwa hiyo miaka miwili na nusu ilikuwa ni kipindi cha kuijenga Yanga, katika kipindi hicho klabu yetu ilikuwa kwenye mazingira magumu, ukizungumzia kifedha ilifikia mpaka wachezaji walikuwa wakivunja mikataba,” anasema Hersi.

Katika mazingira hayo, Hersi anakumbushia kitendo cha beki wao Lamine Moro.

“ Wachezaji walikuwa wanarudi nyumbani na kuvunja mikataba, kama mtakumbuka Desemba 2019 aliyekuwa beki wetu Lamine (Moro) aliondoka na kurejea kwao, Ghana kwa sababu ilikuwa tu hajalipwa stahiki zake na wengine waliamua tu kuachana na Yanga.

“Ukitoka kwa wachezaji kuja kwenye benchi la ufundi nako kulikuwa na changamoto ukija kwenye makazi na kambi ya timu, utaona timu ilikuwa inakaa kwenye hoteli zenye hadhi za chini hakukuwa na mazingira bora, kulikuwa hakuna sehemu maalumu utakayoona klabu inafanyia mazoezi ilikuwa ni maisha ya kuhamahama leo utasikia Chuo cha Polisi siku nyingine Chuo Kikuu kwa klabu kama Yanga haikupaswa kuwa hivyo,” anasema na kuongeza:

“Ukija pia kwenye matokeo bado nako kulikuwa na changamoto kubwa, mahusiano ya klabu na wanachama na mashabiki wao yalikuwa chini sana,” anabainisha Hersi.

“Hatukuwa na uwezo hata wa kujaza uwanja, mlikuwa humuoni timu ikiwapa matumaini mashabiki wao na mashabiki walikuwa wakilalamika juu ya timu. Kwa muktadha huo ulikuwa huioni Yanga iliyokuwa kamili wakati huo tunaingia,” anaongeza:

“Kwanza tukaibadilisha kiuchumi, tukaingia mikataba miwili ya kutengeneza jezi ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kuitengeza klabu ili iwe hata na vifaa vyake ambavyo vingekuwa na manufaa. Wakati huo Yanga haikuwahi kunufaika na hata shilingi moja katika mauzo ya jezi zake.”

Rais huyo wa Yanga anasema kipindi hicho kilikuwa kigumu sana na kilihitaji maarifa na ustahamilivu.

“Hapo tulikuwa tunaizungumzia mwaka 2019 lakini sasa Yanga imeendelea na inanufaika zaidi na biashara ya jezi. Ndani ya utawala wangu Yanga inasaini mkataba mkubwa na wenye thamani wenye thamani ya Sh 9 bilioni. Unaweza ukaona ni kwa kiasi gani klabu imekua kwa kipindi cha miaka mitatu. “Yanga inatoka kuvuna sifuri hadi kufikia kiasi hicho cha fedha, hili sio jambo dogo kuna kazi kubwa sana imefanyika katika kuirudisha hadhi klabu hii. Sasa Yanga inakwenda kuweka rekodi kwa klabu nyingine za Afrika Mashariki kwa kutengeneza fedha nyingi kupitia mauzo ya jezi zake,” alisema.


YANGA IKO SAFI SASA

“Ukiangalia tulipotoka tukaanza kufanya usajili bora wa kikosi chetu hatua kwa hatua ili kurudisha ubora wa timu yetu. Tukaongeza hamasa ya kifedha kwa wachezaji kupitia posho za ushindi wa mechi, timu ikahama kutoka mahotelini na sasa inakaa katika kambi yenye hadhi na inayotambulika na pia tukaboresha benchi la ufundi kutoka mazingira ya makocha waliopita na sasa tuna kocha mwenye leseni ya Pro Diploma ya Uefa, tuna kocha mwenye leseni A ya CAF kama kocha msaidizi, tuna kocha wa makipa bora kutoka Brazil, daktari wa viungo bora kabisa, kocha wa mazoezi ya viungo bora kutoka Tunisia na wataalamu wengine hayo utayapata Yanga ya sasa hivi.”


MABADILIKO YA MFUMO

Kama haitoshi, Hersi anafunguka kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.

“Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji yalishaanza na sasa yanaendelea katika utawala wangu. Tumetangaza nafasi mbalimbali za ajira ambazo zitakwenda kujenga sura mpya ya uongozi, mtaona kuna mfumo wa usajili wa wanachama ulikuwa unaendelea lakini kuna lingine linakuja katika kipindi cha wiki moja au mbili mfumo wa usajili wa mashabiki utazinduliwa,” alisema.


URAIS YANGA uLIPANGA?

“Binafsi siwezi kusema ulikuwa ni uamuzi wa muda mrefu au ni wa kushtukiza hii ilikuwa kama ni wakati ambao Mwenyezi Mungu alipanga iwe hivyo, bahati nzuri kupitia kampuni yangu ya GSM na udhamini pamoja na majukumu yangu yalinifanya nafasi yangu hiyo niwe karibu na Klabu ya Yanga kwa ukaribu zaidi.

“Hatua ya kwanza kwangu ilikuwa ni ile kufanya vizuri katika majukumu ambayo nilikuwa nayafanya wakati huo nikiwa sehemu ya kampuni, inawezekana ikawa haikuwa kwa asilimia 100 lakini kwa kiwango kikubwa nilijituma kwa nguvu na nikaisadidia Yanga kubadilika, ilikuwa ninaposhika jukumu la Yanga fikra na nguvu zangu zote ni kuhakikisha tunafanikiwa kwa kuwa maumivu na furaha yote yalikuwa yananihusu, mwisho yote tukafanikisha kuitangaza kampuni na kuisadia Yanga.

“Ulipokuja uchaguzi kukawa na nafasi ambazo nazipitia nikaona zinanishawishi, kiukweli nguvu nyingine kubwa ilitoka kwa watu wa nje, wanachama, mashabiki na marafiki walinipa ujasiri wakinitaka kugombea hasa wakitaja jinsi nilivyopambana kulisimamia vyema jambo lolote la Yanga, ikafika wakati nikapokea mapendekezo yao na kuangalia nafasi kisha nikajitathimini nikaona natosha kuiongoza Yanga.

Hersi anasema wakati wanaingia Yanga walitoa ahadi za kuibadili Yanga ambazo wengi hawakuamini kama wengeweza kuzitimiza.

“Ukiangalia utaona jinsi tulivyoanza katika utawala huu tulikuwa na ahadi ya kuibadilisha zaidi Yanga kiuchumi na hii mikataba tuliyoanza nayo mtaona jinsi dhamira yetu inavyotekelezeka.

“Na bado mambo mengine zaidi yanakuja lakini sio hivyo tu, dhamira yangu ni kuona Yanga inafanya vizuri uwanjani tunaendelea kupigania ushindi na kucheza kwa ubora na ahadi nyingine kubwa ni suala la ujenzi wa uwanja.

Hersi anasema hili la uwanja ni kiu yake kubwa na anamuomba Mungu alikamilishe katika kipindi cha kwanza cha uongozi wake.

EXCLUSIVE: Hersi atoboa siri, Msola kuitanguliza Yanga iko hivi...

MSOLA ALIITANGULIZA YANGA

Hersi ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM anaeleza jinsi aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msola alivyokuwa kioo kizuri kwake kwa jinsi alivyotanguliza maslahi ya Yanga

“Msola ni mtu muhimu sana kwenye maendeleo ya klabu hii. Aliifungulia milango GSM kuwekeza, alihakikisha malengo ya klabu hii yanafikiwa na hakuweka mbele maslahi binafsi wakati timu hii ilipokuwa inahitaji msaada wa ziada,” anasema.

Rais huyo kijana zaidi kuingoza Yanga anasema Msola amekuwa ni muongozo mkubwa kwenye maeneo ambayo aliona Yanga inahitaji nguvu nyingine.


HALI YA KIFEDHA YANGA IKOJE?

Kuhusu suala la fedha, Hersi anasema mambo ni bado na kusisitiza tena bado sana kwani mahitaji ni makubwa kuliko mapato na wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wanaweza upungufu uliopo.

“Niseme tu klabu ya soka sio tu kuvuka yale malengo unayoyatarajia. Sio kwamba mahitaji yako ni bilioni moja na utafute bilioni moja, la hasha unachotakiwa kufikia bajeti yako, klabu inatakiwa unatengeneza kikubwa zaidi na mahitaji yako yawe madogo ili uweze sasa kufanya vitu vya maendeleo,” anafafanua.

Hapo Hersi anatoa mfano zaidi “Unaweza ukawa unazungumzia ujenzi wa uwanja huwezi ukawa unapata shilingi 1,000 halafu matumizi yako yawe ya shilingi 1,000 na baadaye useme utajenga uwanja. Inatakiwa upate 1,000 matumizi yako yawe shilingi 200 na 800 ikusaidie kufanya mambo ya maendeleo,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa bado hatujafika mahali ambapo tunahitaji 1,000 na tunapata 1,000 tuko chini kuna mapungufu yanayotokana na mapato yetu. Matumizi ni makubwa kuliko mapato, kwa hiyo jitihada zangu ni kuhakikisha kwanza tunavuka kwenye hatua ya kutengeneza hasara ambayo inapatikiana kila mwaka.

Kiongozi huyo ambaye aliyehusika kwenye sajili za wachezaji wengi wa Yanga anasema: “Hivi karibuni tumefanya ukaguzi wa mahesabu ya mwaka 2019-20 imeonyesha klabu inatengeneza hasara. Kwenye hiki kipindi ambacho tunahitaji kutengeneza faida kuna miradi mingi ambayo tunatakiwa tuifanyie kazi,” anasema.

Pia, Hersi anafafanua kuhusu biashara ya soka na jinsi ya kuindesha.

“Moja katika hayo usisahau biashara yako ya mpira ambayo inakufanya kusajili wachezaji wakubwa na uwezo mkubwa zaidi ili walete tofauti chanya kwenye uwanja na ukishafanya hivyo gharama zinaongezeka zaidi.”


MATUMIZI YA YANGA

Mwanapoti linamtaka Hersi kufafanua kuhusu uendeshaji wa klabu na kuweza kupata faida katika biashara.

“Kwanza kwa mfano mwanzoni mwa msimu unahitajika kufanya usajili wa wachezaji. Ili uweze kufanya usajili ulio bora utahitajika kuwa na kiasi kama Sh 1 bilioni mpaka 1.5 bilioni hapo utapata timu imara ambayo itaweza kukusaidia kwenye mashindano.

“Sokoni sasa ukitaka mchezaji bora unatakiwa kuwa na Dola 50,000 mpaka 100, 000 hiyo ni sawa na Shilingi 200 milioni na zaidi.

“Ukiwa na wachezaji watano tu wa namna hiyo unatakiwa kuwa na 1 bilioni bado kikosi chako kinahitaji kuwa na wachezaji 27, utaona hesabu zilivyo hapo, usisahau hao wachezaji kila msimu wana ada zao za usajili kwa hiyo bajeti yako inatakiwa kuwa hivyo, hiyo tu peke yake ni eneo la kwanza la gharama,” anasema Hersi na kuongeza ukishamaliza kuwasajili wachezaji wanahitaji mishahara ya miezi 12 ya kwa msimu.

“Katika hali ya kawaida unahitaji uwe na kiasi cha Shilingi 300 milioni mpaka 400 nne kwa mwezi mmoja ili uweze kumudu kuwalipa hapo utaona hesabu zinakuja uwe na kiasi cha Sh 5 bilioni taza kumudu kulipa mishahara,” anasema.

Kisha anafafanua kwamba ukitoka hapo unatakiwa kuwa fedha za kugharamia kambi kwa msimu mzima,

“Pia unatakiwa kuwa fedha za kuwalipia pango za nyumba hawa wachezaji, hapo wanapofanyia mazoezi kuna gharama zake za kupatunza, vyakula vyao, nyumba zao za kambi, uwalipie ving’amuzi, kuna gharama za safari.

Hersi anatoa mfano timu inatoka Dar es Salaam inakwenda Mwanza, kama msimu uliopita walipokwenda kucheza dhidi ya Geita Gold na baadaye dhidi ya Simba, anasema unahitajika kukaa karibu wiki moja na kuhitaji kiasi kama Shilingi 100 milioni kama bajeti.

“Hapo utalipia chakula, hoteli, usafiri wa ndege kwenda na kurudi na usafiri wa ndani mkiwa Mwanza,” anasema.

Ghafla anakumbuka kitu na kusema “Nisisahau wachezaji watahitaji tiketi za kurudi makwao angalau tiketi moja ya ndege kwa msimu ya kwenda na kurudi.

“Kwa gharama hizo chukua kwa msimu una mechi 30 na kwenye hizo mechi utahitajika kusafiri ugenini kwa asilimia 40 ya mechi hizo na 60 utabaki nyumbani, utaona jinsi gharama zilivyo, hatujaweka posho za wachezaji kama wakishinda.

“Hawa wachezaji wa kigeni wana mahitaji yao mengine kwa kuwa wanacheza mbali na makwao. Pia, kuna ada za usajili, kuna vibali vya kazi kila mchezaji ni Dola 1,000, kibali cha makazi Dola 2,000 ,TFF nayo ina ada yao kila mchezaji Dola 2,000, kuna Baraza la Michezo Dola 500 utaona kila mchezaji unahitaji kuwa na kama Dola 5,500 ili kumuona mchezaji mmoja wa kigeni anavaa jezi na kucheza uwanjani.”

Mbali na hayo Hersi pia anasemabenchi lao la ufundi lina watu wasiozidi wanne tu ambao ni wazawa wengine wote wageni kwahiyo sio kitu rahisi.

Anasema kama alivyosema awali ajenda kuu ni kuijenga Yanga na kuwa imara kiuchumi tofauti na ilivyokuwa. “Tumeshaanza kama hivi mnavyoona, tulisaini mkataba na wadhamini wakuu Sportpesa, baadaye tukasaini mkataba na GSM katika mikataba miwili mikubwa ambayo inahusiana na bidhaa zetu za jezi na vifaa vingine. Tumeingia mkataba na Jackson Group kwa malengo mapana ya kwamba sasa bidhaa zipo zinatakiwa zipigiwe kelele.”

Hersi anasema Yanga ina nafasi ya kumtangaza mtu ili aweze kufikiwa na watu wengi zaidi na Jackson Group wamewapata na wanaamini wanaweza kwenda kuwauza na kuwafikisha mbali.

Hesri anafichukua kuhusu mkataba mwingine ambao Yanga itaingia hivi karibuni na anaamini mkataba huu utakuwa na manufaa makubwa kwa klabu. Mkataba utatoka katika kampuni ya usafirishaji.

“Kuna kampuni kubwa ambayo inatoka nje ya nchi tumeshafika pazuri na mkataba huu utakwenda kutufungulia milango ya wadhamini wengine wakubwa kutoka nje, hii ni kampuni ya kimataifa,” anasema Hersi na kuonekana kujiamini kile alichokuwa akikizungumza.

Anasema akiwa kiongozi ndani ya Yanga anafanya hayo kwa kushirikiana na wenzake ili kuiweka Yanga sehemu salama zaidi.

“Tunafanya hivyo kuhakikisha tunatekeleza yale ambayo wanachama na mashabiki wetu walituamini na kutupa dhamana hii ya kuiongoza hii klabu kubwa ili tuinasue kutoka kwenye mikwamo ya kiuchumi.”

ITAENDELEA KESHO.....