Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu atoa ya moyoni, autaja uongozi Simba

FADLU Pict

Ilikuwa hadithi ya kusadikika na stori za mitandaoni kwa kile ambacho kila shabiki wa Simba alikuwa anakiona kama ndoto kuhusu kuondoka kwa kocha wao Mkuu, Fadlu Davids.

Hatimaye kocha  Fadlu Davids amevunja ukimya baada ya kuwapo kwa taarifa za muda mrefu kuhusu kuondoka Simba na kwenda kujiunga na Raja Athletic, akieleza kila kitu alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi.

Katika mahojiano hayo Fadlu alisema hajaondoka kwa kukurupuka bali alifanya makubaliano na uongozi wa Simba, kuwajulisha ofa aliyokuwa ameipata ya kurejea Raja ambako awali alihudumu kama kocha msaidizi.

Fadlu baada ya kuisimamia Simba katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) ikishinda huko Botswana bao 1-0 dhidi ya Gaborone United, hakurudi na timu Tanzania badala yake aliishia nyumbani kwao Afrika Kusini na kuanza safari ya kwenda Morocco kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Raja.

“Kila hatua ya kuwapo kwa ofa ya kutakiwa na klabu ya Raja niliujulisha uongozi wa Simba, hivyo nimemalizana nao kwa amani na nitaendelea kuheshimu ushirikiano wao kwa kipindi nilichoaminiwa kuifundisha timu na naamini pengine siku moja naweza kurejea,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Naamini nimeacha msingi mzuri ambao utaendelezwa na kocha mwingine atakayekuja nyuma yangu, kuhakikisha Simba inafikia malengo yake kwa msimu huu, naamini itafika mbali katika michuano ya CAF na kupambania ubingwa wa Ligi baada ya msimu uliopita kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo.”


KUHUSU USAJILI

Kocha Fadlu alisema japokuwa aliwakosa baadhi ya wachezaji aliowahitaji kikosini akiwamo Feisal Salum ‘Fei Toto’ (aliyemaliza msimu uliopita na asisti 13 na mabao manne) na kiungo Balla Moussa Conte aliyejiunga na Yanga, alisisitiza Simba bado ina wachezaji wazuri.

“Bado Simba ina kikosi kizuri kitakachoibua ushindani dhidi ya timu pinzania, kikubwa waendelee kujituma na kuzingatia nidhamu ya kazi yao,” alisema Fadlu aliyesisitiza upendo wa mashabiki wa klabu hiyo utaendelea kuishi moyoni mwake.

Fadlu ameondoka na msaidizi wake, Darian Wilken na kocha wa makipa, Wayne Sandilands.

Ndani ya siku 444 sawa na miezi 14 au wiki 63 tangu aajiriwe Julai 5, 2024, Fadlu aliiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni baada ya miaka 31 tangu wekundu wa Msimbazi kucheza fainali ya kwanza katika michuano ya CAF.

Rekodi zinaonyesha kwa siku hizo, Fadlu ameiongoza Simba katika jumla ya mechi 53 za mashi-ndano yote, zikiwamo 30 za Ligi Kuu, 14 za Kombe la Shirikisho Afrika, moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tatu za Ngao ya Jamii na tano za Kombe la Shirikisho (FA).

Katika mechi 30 za Ligi, Fadlu ameshinda 25 kutoka sare tatu na kupoteza mbili, huku akifunga mabao 69 na kufungwa 13 akizoa jumla ya pointi 78, wakati katika mechi tatu za Ngao ya Jamii amepoteza mbili na kushinda moja, Simba ikifunga bao moja na kufungwa mawili.

Kwa Kombe la FA, Simba ilishinda mechi nne kati ya tano, huku moja ikipoteza katika nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars na ilifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa matano, wakati kwa Ligi ya Mabingwa imecheza mechi moja na kushinda kwa bao 1-0.

Kwa Kombe la Shirikisho  Afrika ikifika fainali, Simba ilishinda mechi saba na kupoteza tatu na kupata sare nne ikiwamo ile ya fainali ya mwisho visiwani Zanzibar, huku ikivuna jumla ya mabao 15 na kufungwa 10. Hii ikiwa na maana katika mechi 53, Simba ya Fadlu ilishinda 38, kupoteza nane na sare saba na kufunga jumla ya mabao 101 na kufungwa 30 hadi anaiacha timu hiyo juzi ikiwa Botswana.

Upande wa mashindano ya ndani kwa msimu uliokuwa wa kwanza kwake na aliutumia kuijenga timu, hakupata taji lolote kwani alipoteza Ngao ya Jamii, alishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu nyuma ya Yanga na ilitolewa katika nusu fainali ya Kombe la FA, japo aliifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.

“Mashabiki waendelee kuiunga mkono timu, ina nafasi ya kufanya mambo makubwa katika michuano yote msimu huu,” alisema Fadlu.


WAACHIWA MSALA

Kocha msaidizi, Seleman Matola ambaye amerejea na timu pamoja na kocha wa viungo,  Reidoh Berdien ambaye alisalia nchini kutokana na kutumikia adhabu ya CAF ndio waliochiwa msala kwa sasa na viongozi kuandaa kikosi hicho kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate keshokutwa, Alhamisi.

Pamoja na kuwa kocha wa viungo, Berdien kitaaluma pia ni kocha wa boli hivyo anaweza pia kutoa usaidizi kwa Matola wakati huo viongozi wa Simba wakifanya mchakato wa haraka kumpata kocha mpya ambaye atarithi mikoba ya Fadlu.


VIONGOZI WAMTEGA

Licha ya kwamba uongozi wa Simba umekuwa kimya juu ya kuondoka kwa kocha huyo, lakini chanzo makini kutoka ndani kimesema klabu hiyo inamtega avunje mkataba ili iambulie mkwanja kulingana na mkataba.

Inaelezwa kuwa mkataba wa kocha huyo na Simba ni kwamba yeyote anayevunja anapaswa kulipa fidia ya mshahara wake wa miezi mitatu na hicho ndicho mabosi wa Msimbazi wanamtega Fadlu aamue mwenyewe kuuvunja ailipe klabu.

“Katika mkataba baina ya kocha na klabu ni kwamba kama Simba itauvunja itamlipa mshahara wa miezi mitatu na iwapo ni yeye ataanza kufanya hivyo, pia atalazimika kuilipa klabu miezi mitatu ya kile anacholipwa na hapa ndipo tunaposubiri,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Tulishazungumza naye na kumueleza kama anaondoka auvunje mkataba mwenyewe, lakini bado hajafanya hivyo na tunasubiri kujua kinachoendelea, kwani ni wazi hatuwezi kuwa naye tena kwa hali ilipofikia baada ya mazungumzo yaliyofanyika kumbakisha kushindikana.”