Morocco achukua mikoba ya Fadlu Simba
Muktasari:
- Simba katika mchezo wa marudiano na Gaborone United inahitaji matokeo ya sare au ushindi wa aina yoyote ili iingie raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Dar es Salaam. Simba imetangaza kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ndiye atakuwa Kocha Mkuu wa muda wa timu hiyo wakati ikisaka Kocha mpya.
Na Morocco atakuwa na kibarua cha kuiongoza Simba katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, Jumapili ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Simba imefafanua kuwa Morocco ataiongoza Simba katika mchezo huo kutokana na kocha aliyepo, Selemani Matola kuwa na adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mchezo wa kwanza, Jumamosi iliyopita.
“Klabu ya Simba inamtangaza, Hemed Suleiman maarufu Morocco kuwa Kocha wa muda 'Caretaker’ wa Klabu yetu kwenye mechi za Kimataifa baada ya Kocha, Fadlu Davids kusitisha mkataba na Kocha Selemani Matola kuwa na kadi nyekundu.
“Uongozi wa klabu unalishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kumruhusu Kocha Morocco ambae ni Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania kujiunga nasi katika kipindi hiki ambacho Klabu inakamilisha taratibu na mchakato wa Kocha wa kudumu wa Klabu yetu.
“Kocha Morocco ataliongoza benchi la ufundi kuelekea Mchezo wa Marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United FC Septemba 28, 2025,” imefafanua taarifa ya Simba.
Simba kwa sasa imebaki na Matola tu baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu Fadlu Davids na wasaidizi wake wanne kutimkia Raja Casablanca ambako wametangazwa rasmi leo.
Morocco anajiunga na Simba akiwa ametoka kuiongoza timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024.
Msaidizi wa Fadlu aaga
Katika hatua nyingine, kocha Darien Wilken ambaye ni miongoni mwa wasaidizi ambao Fadlu amejiunga nao Raja Casablanca, ameiaga klabu ya Simba na kuishukuru.
“Sio rahisi kusema kwaheri hasa kwa klabu ya kipekee kama Simba. Kwa muda niliofanya kazi hapa nimepata kipaumbele cha kufanya kazi sio tu na wachezaji wazuri bali pia klabu nzima, na jumuiya inayopumua shauku, uvumilivu na matarajio.
“Kwa klabu na mashabiki wake nawashukuru kwa imani mliyoweka kwangu na mapokezi mazuri ambayo nilipata. Simba ni zaidi ya timu, ni familia na kuwa sehemu ya familia hii kumekuwa ni uzoefu ambao nitaubeba daima.
“Ninapopiga hatua nyingine katika njia yangu, naondoka bila kingine zaidi ya heshima na thamani tuliyoipata pamoja. Daima ni fahari kuwa sehemu ya Simba na nitaendelea kuifuata na kuisapoti klabu yenye matarajio makubwa,” ameandika Wilken.