Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FBI, Polisi Marekani wajitosa nusu fainali Argentina na England

Muktasari:

  • Mchezo wa Jumatano utakuwa wa 15 kuzikutanisha timu hizo katika mashindano tofauti huku ukiwa wa sita kuzikutanisha katika Kombe la Dunia.

Mamlaka za usalama Marekani, FBI na Idara ya Polisi zimekutana na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa ajili ya kupanga mikakati ya kiusalama kwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya Argentina na England utakaochezwa kesho Jumatano, Julai 15, 2026 saa 5:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Mechi hiyo inatazamwa kama yenye tishio kubwa zaidi la kiusalama kwa mashabiki na watu binafsi kutokana na uhasama uliopo baina ya timu hizo mbili.

Sababu kubwa inayotajwa kuchochea uhasama baina ya timu hizo ni ugomvi wa kuwania visiwa vya Falklands kati ya mataifa ya England na Argentina.

Chanzo cha uhasama huo wa kihistoria ni vita ya Falklands iliyopiganwa mwaka 1982 kuwania visiwa hivyo vilivyo chini ya England kwa sasa huku Argentina ikiendelea kusisitiza kuwa ni mali yake.

Ipo video inayoonyesha wachezaji na mashabiki wa Argentina wakiimba nyimbo zinazoihusu England na visiwa hivyo.

Na kingine kinachokoleza uhasama baina ya timu hizo mbili ni tukio la mwaka 1986 ambapo hayati Diego Maradona alifunga bao kwa mkono lililopewa jina la utani la Mkono wa Mungu, katika mechi ambayo England ilifungwa mabao 2-1 na Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.

Wakati dunia ikisubiri mechi hiyo, tayari imeripotiwa vurugu zimeanza kujitokeza kwa mashabiki wa timu hizo jijini Miami baada ya mechi ya robo fainali baina ya England na Norway.

Miongoni mwa hatua ambazo FBI na Polisi Marekani wamepanga kuzichukua ni  kuongeza idadi ya walinzi wa usalama ili kuendana na umati wa mashabiki wa timu hizo.

Pia imepangwa kwamba mashabiki wa timu hizo watatenganishwa katika ukaaji majukwaani badala ya kujichanganya pamoja kama ilivyo katika mechi nyingine.

Taarifa ya idara ya Polisi jijini Atalanta, imesema kuwa hatua hizo za kiusalama hazitoishia uwanjani tu.

“Wataalam wa ziada na rasilimali zimeshaanza kutumika na zitaendelea kupangiliwa kistratejia ndani na maeneo ya karibu ya uwanja ambako tukio linafanyika, maeneo ya starehe na yale yenye msongamano mkubwa wa watu kusaidia kuhakikisha usalama na mazingira ya furaha kwa kila mmoja,” imefafanua taarifa hiyo ya polisi.

Mchezo wa Jumatano utakuwa wa 15 kuzikutanisha timu hizo katika mashindano tofauti huku ukiwa wa sita kuzikutanisha katika Kombe la Dunia.

Katika mechi 14 ambazo timu hizo zimekutana hapo nyuma, England imepata ushindi mara sita, sare ni tano na Argentina imeshinda mechi tatu.